Home Habari za usajili Bongo MASHABIKI WA SIMBA & YANGA WAMKALIA KOONI CHAMA

MASHABIKI WA SIMBA & YANGA WAMKALIA KOONI CHAMA

Habari za Usajili

WAKATI wachambuzi na waandishi wa habari za michezo wakiendelea kutoa taarifa kuhusu hatma ya Clatous Chama Simba, mashabiki wa Simba na Yanga nao hawapo nyuma, wamefunguka mengi kuhusu mchezaji huyo.

Mkataba wa Chama Simba unamalizika Jumapili Juni 3, hivyo anahusishwa zaidi kujiunga Yanga kama Simba hawatompatia maslahi mazuri zaidi.

Shabiki wa Yanga, Azizi Kalinga, alisema kiungo huyo ni mmoja wa wachezaji wenye uwezo mkubwa kwa sasa na hakuna timu ambayo ikifanikiwa kumpata itajutia usajili huo.

Kalinga alisema mchezaji huyo ana uzoefu na amekuwa akisaidia timu yake kupata matokeo muhimu na hiyo inatokana na kipaji alichonacho.

“Sisi tumejipanga na tumekamilika, tuna uwezo wa kumpata mchezaji yoyote tunayemhitaji hapa Tanzania, hatutamkosa, iwe Clatous Chama au Prince Dube, hatuwezi kushindwa kumsajili ,” alisema shabiki huyo.

Amri Diaz, alisema anaamini walifanikiwa kumnasa Chama, kikosi chao kitakuwa imara na kitatoa ‘dozi’ kwa kila watakayekutana naye.

“Naona kabisa kuna mtu atakula 10 msimu ujao, huku Chama huku Dube, tutakuwa na kikosi tishio Afrika, tunaamini hakuna atakayeweza kututisha, hakuna atakayeingia mguu wake akatoka salama,” alitamba shabiki huyo wa Yanga.

Aliongeza lengo la Yanga kusajili wachezaji mbalimbali ambao ni mahiri na wazoefu ni kutaka kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kufanya vyema kwenye mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Naye mwanachama wa Simba, Fadhila Juma, alisema bado Chama ni mchezaji muhimu ambaye anahitajika ndani ya kikosi chao.

Alisema kumwacha Chama kwa sasa hautakuwa uamuzi wa busara kwa sababu timu yao inahitaji kuimarishwa katika idara zenye mapungufu.

“Kumwacha Chama si uamuzi mzuri, kwa upande wangu naona bado ana nafasi na mchango mkubwa katika kikosi chetu, kwa sasa unaweza kuleta mtu mpya, je kama atashindwa kuonyesha uwezo wake au kuingia katika mfumo itakuaje, itaigharimu timu,” alisema shabiki huyo.

SOMA NA HII  ILE ISHU YA SAOTHAMPTON YA UINGEREZA KUTAKA KUMSAJILI MTZ NOVATUS IKO HIVI....