Home Habari za Usajili Yanga SABABU 5 YANGA KUINGILIA DILI LA SIMBA KWA MWAMNYETO

SABABU 5 YANGA KUINGILIA DILI LA SIMBA KWA MWAMNYETO

habari za Yanga

INAELEZWA kuwa kuna sababu 5 zilizowafanya Mabosi wa Yanga kumpatia mkataa mpya wa miaka miwili, kitasa Bakari Mwamnyeto, ambapo mwanzoni watani zao walikuwa wanakaribia kuinasa saini ya mchezaji huyo.

Mwamnyeto aliyetua Yanga Agosti 2020 akitokea Coastal Union, mkataba wake na Yanga ulikuwa unamalizika Juni 30, mwaka huu, hivyo alibakisha takribani siku nne awe huru kabla ya kusaini dili jipya.

Ili Yanga kufanikisha kumpa beki huyo mzawa mkataba mpya wa miaka miwili zimewatoka Sh300 milioni zikiwa ni pesa ya usajili huo.

Hapa kuna sababu tano zilizowafanya Yanga kuendelea kuwa na beki huyo. Kuhofia kuwaachia Simba mali.

Hofu ya Simba SC

Yanga walikaa chini na kufikiria mara mbili kwamba Mwamnyeto akiondoka kisha akatua kwa wapinzani wao hali itakuwaje, jibu walilopata moja kwa moja likawafanya wampe mkataba fasta.

Hilo lilikuja baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba endapo Mwamnyeto atashindwana na Yanga katika ishu ya mkataba mpya, basi Simba walikuwa tayari kumchukua. Yanga wakaona siyo kweli, acha tubaki na mali yetu kwani wakiiachia inaweza kuwa pigo kubwa kwao pindi akitua kwa wapinzani.

Nani Kurithi Nafasi Yake.

Kumkosa mridhi wake Yanga wameangalia akiondoka Mwamnyeto katika eneo la ulinzi wa kati nani atakuja kuchukua nafasi yake kwa mabeki wazawa waliopo hivi sasa.

Ukiangalia katika timu kubwa za Simba, Yanga na Azam kwa msimu uliopita, Yanga pekee ndiyo ina mabeki wengi wa kati wazawa wanaocheza kikosi cha kwanza, timu zingine zinawatumia wageni au mchanganyiko. Yanga wanaweza kumpanga Job na Bacca ambao wote wazawa huku benchi akikaa Gift Fred kutoka Uganda na Mwamnyeto mwenyewe.

Pale Simba, Henock Inonga na Che Malone Fondoh ndiyo walijenga utawala wao, hawa wote ni raia wa kigeni, wazawa Kennedy Juma na Hussein Kazi walibaki nje kuwaangalia wenzao.

Azam tangu amekuja Mcolombia, Yeison Fuentes, amekuwa na uhakika wa namba kikosi cha kwanza akicheza sambamba na Mkongomani, Yannick Bangala.

Uzoefu Wake

Uzoefu Kwa kipindi chote cha misimu minne alichochezea Yanga, Mwamnyeto amekuwa miongoni mwa wazawa waliokuwa wakipata namba chini ya makocha waliomnoa Zlatko Krmpotic, Cedric Kaze, Juma Mwambusi kabla ya kupokewa na Nasreddine Nabi na Miguel Gamondi.

Pia hata katika timu ya taifa, Taifa Stars nyota huyo amekuwa akiitumikia mara kwa mara akifanikiwa kwenda Ivory Coast kushiriki michuano ya Afcon 2022.

Hiyo yote inamfanya kuwa miongoni mwa mabeki wazawa wenye uzoefu mkubwa ndani ya uwanja ukizingatia kwamba ni kiongozi wa timu.

Umbo Lake Kiuchezaji.

Kimo kinambeba Kwa wastani, kimo cha beki wa kati angalau inatakiwa kuwa urefu wa mita 1.80 mpaka 1.88 na kuendelea ili kukabiliana vizuri na washambuliaji ambao nao wastani wao huwa mita 1.86.

Kwa upande wa Mwamnyeto yeye ana urefu wa mita 1.85 hivyo unamfanya kuwa ni beki aliyefuzu viwango kwa upande huo wa kimo. Licha ya kwamba urefu ni kigezo kikubwa cha beki wa kati, lakini pia bila ya juhudi binafsi katika kuonyesha uwezo ni kazi bure.

Ndani ya Yanga, Bacca mwenye urefu wa mita 1.77 na Job (1.68) ndiyo wamepata muda mwingi wa kucheza msimu uliopita, huku Mwamnyeto akiishia nje, hiyo ilitokana na kushuka kiwango kidogo.

Kusaidia Ushambuliaji.

Kusaidia kushambulia Licha ya kwamba Mwamnyeto ni beki wa kati, lakini ana uwezo wa kubadilika kulingana na hali ya mchezo inavyokwenda.

Msimu wa 2022-23 wakati Yanga inafanikiwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, alikuwa sehemu ya waliotengeneza mabao ya timu yake.

Katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Rivers United uliochezwa nchini Nigeria ukiwa ni wa marudiano, Yanga ilishinda 2-0 na kufuzu nusu fainali baada ya nyumbani kutoka 0-0.

Mabao hayo yote yalifungwa na Fiston Mayele dakika ya 74 na 81 huku Mwamnyeto akifanikiwa kutoa asisti zote mbili. Kwa kifupi, Yanga ilikwenda nusu fainali Mwamnyeto akiwa sehemu ya wachezaji muhimu wa kupatikana kwa mabao hayo. Msimu huo pia alifunga mabao mawili ligi kuu.

Mbali na hilo, beki huyo pia mara kwa mara anapopata nafasi ya kucheza, amekuwa akienda mbele kuongeza mashambulizi wakati wa upigwaji wa kona au hata faulo kwa wapinzani, kitu hicho kimemfanya awe na mabao matano katika ligi kuu tangu atue Yanga.

Mwamnyeto aliyekitumikia kikosi hicho kwa misimu minne huku mitatu mfululizo ikiwa na mafanikio makubwa kwake na timu akiwa nahodha, sasa anaendelea kuwa sehemu ya timu hiyo ambayo msimu ujao itakuwa na jukumu la kutetea makombe mawili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).

SOMA NA HII  TEGETE AWACHANA MAKAVU YANGA..."ACHENI DHARAU"...AMEZUNGUMZA HAYA