Home Habari za Simba Leo KOCHA MPYA AZUIA KAMBI YA SIMBA…KUANZA RASMI J3

KOCHA MPYA AZUIA KAMBI YA SIMBA…KUANZA RASMI J3

Habari za Simba leo

RATIBA ya Simba kwa wachezaji kuanza kuripoti kambini kabla ya kusafiri kwenda Misri ilitakiwa kuanza Juni 27, kabla ya kikao cha leo cha wachezaji wote, benchi la fundi na Muwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mohammed Dewji.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema, kambi ya Simba ya kulikusanya jeshi jipya sasa itaanza rasmi Jumatatu (Julai Mosi), ikielezwa inasubiriwa kutangazwa kabisa kwa kocha mkuu mpya wa kuisimamia timu kabla ya kusafiri kwenda Misri kujiandaa na msimu mpya wa mashindano.

Inaelezwa ishu ya kocha mkuu ndio imefanya mabosi kuwapa taarifa wachezaji wote kwamba watakutana Jumatatu, kwani benchi nzima la ufundi nalo litakuwa tayari kuja kufanya kazi na sasa ingekuwa ngumu kuita wachezaji bila ya kuwa na kocha ambaye anapaswa kutambulishwa kabla ya timu kusafiri hadi Misri.

Simba sasa imepanga kuanzia Julai Mosi wachezaji na benchi zima la ufundi kuanza kuwasili kambini jijini Dar kuweka mambo sawa kujiandaa na kambi yao ya maandalizi ya msimu ujao ‘pre season’ inatarajiwa kuanza rasmi Julai 8 mwaka huu huko nchini Misri.

Baada ya kukutana Julai Mosi, zoezi litakalofanyika ni wachezaji wote kufanyiwa vipimo vya afya kuanzia wale wapya waliosajiliwa kipindi hiki na waliokuwepo msimu uliopita.

“Kambi yetu rasmi ya kujiandaa na msimu ujao inaanza Julai Mosi mwaka huu ambapo wachezaji na makocha wote wanatakiwa kufika kambini kwa ajili ya maandalizi ya safari,” alisema mtoa taarifa na kuendelea.

“Baada ya kufika kila mmoja, litafanyika zoezi la upimaji afya kwa wachezaji wapya na wale wa zamani.”

Mtoa taarifa huyo aliendelea kubainisha kwamba baada ya vipimo vya afya kumalizika, wachezaji watagaiwa vifaa vyao vya mazoezi.

“Kila mchezaji atakabidhiwa vifaa vyake vya mazoezi baada ya kumalizima kupima afya, kisha safari yetu itakuwa Julai 8 kuelekea Misri kuweka kambi yetu,” alisema chanzo hicho, huku mtu mwingine wa karibu wa klabu hiyo alidokeza ishu ya kocha mkuu mpya ni kingine kilichokwamisha kwa sasa.

Simba haina kocha mkuu rasmi, tangu alipoondoka Abdulhak Benchikha na nafasi yake kukaimiwa na Juma Mgunda anayeelezwa ameshamaliza mkataba na klabu hiyo na mchakato unaelezwa upo pazuri, huku jina la Steve Komphela kutoka Afrika Kusini likitajwa sambamba na kusakwa na makocha wa makipa, wa mazoezi.

Simba imepanga kuweka kambi Misri kwa takribani wiki tatu kabla ya kurejea nchini kujiandaa na Tamasha la Simba Day sambamba na michezo ya Ngao ya Jamii itakayoanza Agosti 8-11 mwaka huu.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amezungumzia kambi yao ya maandalizi ya msimu ujao akisema: “Tunatarajia kwenda Misri katika Mji wa Ismailia kuweka kambi ya maandalizi ya msimu ujao.

“Tumechagua kwenda Misri kwa sababu hali ya hewa ni rafiki kwetu lakini pia timu nyingi zinakwenda huko hasa katika Mji wa Ismailia kutokana na utulivu uliopo kulinganisha na Cairo kwenye hekaheka nyingi. Tunatarajia kuondoka wiki ya kwanza ya mwezi Julai kwenda huko kuweka kambi.”

SOMA NA HII  BAADA YA KUTOLEWA LIGI YA MABINGWA AFRIKA....SIMBA SC WAAPA KUIHARIBIA YANGA SC...