Home Habari za michezo MOROCCO…STARS IPO KAMILI KUIVAA ETHIOPIA

MOROCCO…STARS IPO KAMILI KUIVAA ETHIOPIA

taifa stars

KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars‘, Hemed Suleimani ‘Morocco’ amesema, kikosi hicho kiko kamili kwa ajili ya michezo miwili ya kimataifa kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), itakayofanyika mwakani.

Stars iliyopo kundi ‘H’ la kutafuta nafasi ya kufuzu michuano hiyo, itashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Septemba 4 mwaka huu kucheza na Ethiopia kisha kuifuata Guinea katika mchezo wa pili utakaopigwa Septemba 10.

Akizungumzia maandalizi ya michezo hiyo miwili, Morocco alisema, wachezaji wote wako katika morali ya hali ya juu huku taarifa za madaktari wa kikosi hicho zikionyesha hakuna mchezaji yeyote ambaye ni majeruhi tangu wameingia kambini.

“Tunaendelea na maandalizi kwa ajili ya michezo hiyo miwili ambayo tunahitaji kufanya vizuri ili kutengeneza mazingira mazuri katika kundi letu, wachezaji wengi hapa ni wazoefu na mashindano hayo, hivyo hatuna hofu juu ya hilo,” alisema.

Kwa upande wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Cliford Ndimbo alisema, wachezaji wote wameshawasili kambini, isipokuwa baadhi tu kwa wale wa Yanga ambao walikuwa Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Wachezaji wa Yanga walioitwa katika kikosi hicho ni kipa, Aboutwalib Mshery, mabeki, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Bakari Mwamnyeto na Nickson Kibabage na kiungo, Mudathir Yahya huku mshambuliaji pekee akiwa ni nyota, Clement Mzize.

Stars iliyopo kundi ‘H’ iko na timu za Ethiopia, Guinea na DR Congo, inawania tiketi ya kufuzu AFCON ambayo itafanyika mwakani Morocco.

Timu hiyo imeshiriki AFCON tatu tofauti ambapo kwa mara ya kwanza ilikuwa ya Nigeria mwaka 1980, kisha ikapata nafasi hiyo tena baada ya miaka 39, ya kushiriki ilipofanya hivyo mwaka 2019, Misri chini ya Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike.

Mara ya tatu ilikuwa mwaka huu wa 2024 kule Ivory Coast ikiwa na Kocha Mkuu, Adel Amrouche ambapo ilipangwa kundi ‘F’ lililokuwa na timu za taifa za Morocco, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kuishia hatua ya makundi.

SOMA NA HII  YANGA YATUA KWA MAKUNDI ETHIOPIA...WAHABESHI WAINGIA UBARIDI