Home Habari za Simba Leo AZAM FC WAIPELEKA SIMBA ZENJI

AZAM FC WAIPELEKA SIMBA ZENJI

Habari za Simba

MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya wenyeji Azam FC dhidi ya Simba uliopangwa kufanyika Septemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, kwa sasa utachezwa Uwanja wa New Complex Amaan Zanzibar kuanzia saa 2:30 usiku.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi (TPLB) jana kupitia kwa Ofisa Habari na Mawasiliano, Karim Boimanda, imeonyesha mabadiliko hayo ya uwanja na muda kwani hapo awali mchezo huo ambao hutambulika kwa ‘Dabi ya Mzizima’ ulipangwa kuchezwa saa 12:00 jioni.

Azam ambao ni wenyeji wa mchezo huo itakutana na Simba iliyo chini ya kocha Fadlu Davids aliyeshinda michezo zote mbili za Ligi Kuu hadi sasa dhidi ya Tabora United kwa mabao 3-0 kisha Fountain Gate 4-0.

Kwa upande wa Azam, iliyo chini ya kocha mpya raia wa Morocco, Rachid Taoussi, ilianza Ligi Kuu Bara kwa suluhu mbili mfululizo dhidi JKT Tanzania na Pamba Jiji, kisha kuzinduka mbele ya KMC kwa kuichapa mabao 4-0 na hilo litakuwa pambano la kwanza kwa makocha wote katika dabi hiyo ya Mzizima.

Mchezo wa mwisho kwa timu hizo uliopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan visiwani Zanzibar, ulikuwa wa fainali ya Kombe la Muungano siku ya Aprili 27 mwaka huu na Simba kushinda bao 1-0, lililofungwa na nyota wa zamani wa kikosi hicho, Babacar Sarr.

Katika Ligi Kuu Bara, mchezo wa mwisho kwa miamba hiyo kukutana ulipigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Mei 9, mwaka huu ambapo Simba iliibuka kidedea kwa mabao 3-0, yaliyofungwa na Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma na David Kameta ‘Duchu’.

Sababu za kuhamishiwa kwa mchezo huo umeingia katika kanuni ya Ligi inayotoa nafasi mbili kwa kila klabu kuchangua mechi mbili za nyumbani kuchezwa nje ya uwanja inayoutumia kwa ligi hiyo, ambapo sio mara ya kwanza kwa dabi kuhamishwa uwanja, kwani msimu uliopita Simba iliipeleka Azam kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na pambano hilo kuisha kwa sare ya 1-1.

SOMA NA HII  WAKATI MBRAZILI SIMBA AKISUBIRI MUDA UFIKE...KOCHA AL AHLY AANZA KUWEWESEKA...