Home Habari za Simba Leo FADLU AAPA KUWAMALIZA WALIBYA…MASHABIKI WAONYWA

FADLU AAPA KUWAMALIZA WALIBYA…MASHABIKI WAONYWA

HABARI ZA SIMBA-FADLU

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema kwa mchezo wa leo hawana kitu kingine cha kufanya zaidi ya kushinda na kufuzu makundi.

Fadlu amebainisha, watatumia mbinu zote za kimchezo kufikia malengo, huku akiwataka mashabiki kutofanya jambo la tofauti na kuwapa sapoti wachezaji wa Simba.

“Kitu kizuri ni kwamba tumefahamu namna mechi waliyotupa ugenini, malengo yetu ya kwanza yalikuwa ni kutoruhusu bao, tukafanikiwa, lakini tulihitaji kufunga ingawa haikuwa hivyo,” alisema Fadlu na kuongeza;

“Kwa sasa tunapaswa kucheza kwa umakini mkubwa, tusiruhusu bao kwani tukiruhusu tunapaswa kufunga mawili ili kufikia malengo. Matarajio ni kufanya vizuri mchezo huu na kufuzu hatua ya makundi, hakuna kingine.

“Malengo ni kushinda mechi na kufuzu, kucheza nyuma ya mpira ni mbinu ya kimchezo lakini tunachokiangalia kesho ni kufuzu sio kingine. Wachezaji wanafahamu ni namna gani tunakwenda kucheza mchezo huu kutokana na tulivyofanya mazoezini.”

AONYA MASHABIKI

Kutokana na kile kilichotokea Libya baada ya vurugu kubwa zilizofanywa na wenyeji mchezo ulipomalizika, Fadlu amewataka mashabiki wa Simba kutofanya kitu cha tofauti zaidi ya kuishangilia timu yao.

“Sitarajii kuona mashabiki wakifanya kitu cha tofauti kwa wageni wetu bali natarajia mashabiki watakuwa nyuma yetu katika kutupa sapoti tunapokuwa na mpira na hata tusipokuwa nao, naamini hawatatuacha peke yetu,”

Alisema Fadlu aliyebainisha kuwa, leo atakosa huduma ya kiungo Mzamiru Yassin anayesumbuliwa na maumivu ya mguu huku matarajio yake ni kuona nyota huyo akirejea kikosini wiki ijayo.

“Mzamiru tutamkosa kwani ana maumivu ya mguu aliyoyapata katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal, naamini wiki ijayo atarudi mazoezini akiwa fiti. Lakini wachezaji wengine wapo,” alisema Fadlu na kuongeza:

“Presha ya mchezo inaweza kuwepo lakini ni namna gani unaweza kukabiliana nayo, kocha unapaswa kuwasaidia wachezaji kuondokana na hiyo presha kwani tunahitaji wao kucheza vizuri. Tunafahamu kwamba matarajio makubwa sio kufuzu tu makundi bali kuchukua na ubingwa pia, hivyo lazima kuwe na presha.”

Kwa upande wa nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, akizungumza kwa niaba ya wachezaji alisema mchezo wa leo ni muhimu kwao na kwamba wamepata muda wa kuzungumza ili kupeana morali.

SOMA NA HII  SABABU MECHI ZA LIGI KUU KUTOTUMIA VAR