Home Habari za Simba Leo FADLU: SIMBA INAENDA KUWA TISHIO

FADLU: SIMBA INAENDA KUWA TISHIO

habari za simba-fadlu

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amewaambia wanachama na mashabiki wa timu hiyo ambao wanaonekana kuanza kukisifia kikosi chao baada ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kuwa bado hakijafika pale ambapo yeye anahitaji, akiwaahidi kuwa baadaye kitakuwa tishio zaidi ya hivi wanavyokiona.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa mkondo wa pili wa raundi ya kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya, Fadlu alisema kikosi chake hakijaimarika vile ambavyo anahitaji, lakini akiwasifu wachezaji wake vijana wasio na uzoefu wa michuano mikubwa kwa kupambana kwa moyo wa kijasiri mpaka kutinga hatua hiyo.

Katika mchezo huo uliochezwa juzi, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba ilishinda mabao 3-1 yaliyowekwa wavuni na Kibu Denis, Leonel Ateba na Edwin Balua, yakiipeleka hatua ya makundi kwa jumla ya mabao hayo, baada ya mchezo wa kwanza ugenini nchini Libya timu hizo kutoka suluhu.

“Tuliruhusu bao, lakini wachezaji wangu hawakuondoka kwenye mpango mkakati, hata wakati wa mapumziko niliwaambia wasiwe na hofu, waendelee kucheza kama ilivyokuwa awali.

Nina kikosi kipya, wachezaji wengi vijana ni mara ya kwanza kucheza hatua hii, nadhani wamejifunza mengi, namna ya kucheza mechi ugenini, mashabiki wanavyojazana uwanjani na kuwazomea, na vituko vya timu za Afrika Kaskazini,” alisema kocha huyo.

Alisema baada ya kutinga hatua hiyo wachezaji wake hasa wale wasio na uzoefu ambao ni wengi kwenye kikosi chake, wataendelea kujifunza hasa kwenye michezo ya makundi, lakini akisema anaendelea kukisuka kikosi chake kuwa tishio.

“Hapa bado, hiki kikosi bado naendelea kukisuka ili kiwe hatari zaidi, naona mashabiki wameanza kuwa na furaha, lakini mimi kama mwalimu bado nina kazi ya kufanya, kitakapofika pale ambapo nahitaji, kitakuwa hakishikiki,” alisema raia huyo wa Afrika Kusini.

Wakati kocha huyo akiongea hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, rais wa Heshima na Mwekezaji, Mohamed Dewji, amewasifia wachezaji wa timu hiyo, akisema kwa sasa wana wachezaji wapambanaji wanaopigania nembo ya klabu.

“Tumepitia miaka michache migumu Simba, lakini ushindi wa leo umenifurahisha sana. Vijana ni wapya na wachanga, lakini wamepigana kwa moyo wao wote,” alisema Mo.

Mchezaji Kibu Denis yeye alionesha kushangaa mabao yake mengi kuyafunga upande wa Kusini mwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, akisema ana bahati nalo.

Kibu aliyefunga bao la kwanza katika mchezo huo, amesema katika kumbukumbu zake amewahi kufunga bao moja tu lango la Kaskazini mwa uwanja huo.

“Yaani mimi huwa nafunga sana kule sijui kwa nini, mabao zaidi ya manane nimefunga upande wa Kusini, katika kumbukumbu zangu nadhani ni bao moja tu nimefunga upande mwingine, hata mechi na Yanga kule kule,” alisema.

Mchezaji na kocha wa zamani, Abdallah Kibaden, yeye alikoshwa na golikipa, Moussa Camara.

“Wasiwasi wangu ulikuwa golini, lakini kumbe tuna kipa mzuri zaidi kuliko wote waliotangulia,” alisema.

SOMA NA HII  SIMBA WAMESHINDA NJE YA UWANJA....SIMBA DAY KUNOGA

1 COMMENT

  1. […] wa Simba SC, Fadlu Davids, amethibitisha kuwa atawakosa nyota wake watatu muhimu katika mchezo […]

Comments are closed.