Home Habari za michezo TAIFA STARS YAAPA KUKIWASHA GUINEA…KUUFUZU AFCON

TAIFA STARS YAAPA KUKIWASHA GUINEA…KUUFUZU AFCON

HABARI ZA MICHEZO-TAIFA STARS

BAADA ya juzi kushindwa kupata ushindi kwenye mchezo wao wa kwanza wa kufuzu fainali za Afrika (AFCON) 2025 dhidi ya Ethiopia, wachezaji wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ wameapa kwenda ‘kukiwasha’ na kupata pointi tatu kwenye mchezo ujao dhidi ya Guinea.

Stars juzi ikiwa nyumbani ilishindwa kupata ushindi kwenye mchezo huo na kulazimishwa kutoka bila kufungana kwenye Uwanja wa Taifa.

Beki wa kati wa timu hiyo, Dickson Job, alisema matokeo waliyoyapata hawakuyakusudia lakini anaamini benchi la ufundi limeona mapungufu yaliyojitokeza na watayafanyia kazi.

“Tulijipanga kupata ushindi, lakini kwa bahati mbaya matokeo ndio hayo, benchi la ufundi litafanyia kazi pale wanapoona hatukufanya vizuri,” alisema Job.

Aidha, alisema mchezo ujao ambao watacheza ugenini wataenda kupambana na kuhakikisha wanapata pointi tatu ili kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi.

Beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohamed Hussein, alisema matokeo ya juzi hayajawakatisha tamaa na wanakwenda kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao.

“Tulitarajia ushindi, lakini mpira una matokeo ya aina tatu, kushinda, kutoka sare au kufungwa, tunaenda kujiandaa kwa mchezo ujao ambapo naamini tutapambana zaidi na kupata ushindi,” alisema nahodha huyo wa klabu ya Simba.

Nahodha wa Stars katika mchezo wa juzi, Himid Mao, alisema licha ya pointi moja waliyoipata, matokeo hayo yamewapa hamasa ya kufanya vizuri zaidi kwenye mchezo unaofuata.

“Tulijitahidi kupambana, lakini wapinzani wetu nao walijitahidi kuonyesha uwezo wao, matokeo haya kwetu ni chachu na hamasa ya kupambana zaidi kwenye mchezo ujao,” alisema Mao.

Kocha wa timu hiyo, Hemed Moroco, alisema Ethiopia ni timu ngumu na walicheza vizuri ndio maana walipata matokeo hayo waliyoyapata.

Alisema licha ya kupambana, walipata upinzani mzuri kutoka kwa wageni wao hao.

Mchezo unaofuata Stars watacheza ugenini, Guinea Septemba 10 huku Ethiopia wakipambana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

SOMA NA HII  KAPOMBE:- LEO KAZI NI MBILI TU...