Home Habari za michezo KUHUSU CHE MALONE KUONGEZA MKATABA SIMBA…UKWELI HUU HAPA….MABOSI WALIGOMA….

KUHUSU CHE MALONE KUONGEZA MKATABA SIMBA…UKWELI HUU HAPA….MABOSI WALIGOMA….

Habari za Simba leo

MABOSI wa Simba wamemaliza utata baada ya kudaiwa kumpa mkataba wa miaka miwili beki wa kati raia wa Cameroon, Che Fondoh Malone wenye masharti.

Beki huyo amepewa mkataba huo wiki kadhaa  ambapo baadhi ya mabosi wa Simba walikuwa wamegawanyika kuhusu kumuongezea beki huyo mkataba mpya au la.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ni kwamba mabosi wa Simba wamekubaliana kumtengenezea mkataba mpya mchezaji huyo, hivyo muda wowote kuanza sasa inatarajiwa kutangaza rasmi kuwa Che Malone ataendelea kuwa sehemu ya familia ya Msimbazi.

Awali, kulikuwa na wasiwasi kutokana na sababu ya kushuka kwa kiwango chake kwenye mechi kadhaa, jambo ambalo lilifanya viongozi wa klabu kutofautiana, lakini kwa haraka na kwa busara, viongozi wa Simba walitambua mchango wa Malone kwa timu wakitambua pia ni mmoja ya mabeki bora wa kati na wa kuaminika wanaoweza kuendelea kuleta faida kubwa kwa timu kwa sasa na miaka ijayo.

“Ni kweli Che Malone ameshapewa mkataba mpya kwa miaka miwili, kilichobaki ni kutambulishwa tu kwa mashabiki, ni beki muhimu kwa kikosi hiki,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Simba.

Mkataba huu mpya ni ishara ya imani kubwa kwa beki huyo, ikionyesha Simba inataka kumweka kama sehemu ya mipango yake ya baadaye, pia ni ishara ya kujenga timu imara yenye wachezaji wenye uzoefu na uwezo wa kushinda, hasa katika michuano mikubwa ya Ligi Kuu na mashindano mengine ya kimataifa.

Che Malone alitua Msimbazi misimu miwili iliyopita akitokea CotonSport ya Cameroon na kutengeneza ukuta mgumu sambamba na Henock Inonga aliyetimka klabuni hapo na sasa akishirikiana na Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue iliyoifanya Simba kuwa wagumu kufungika katika Ligi Kuu.

Hadi sasa Simba ndio timu iliyoruhusu mabao machache katika ligi ikifungwa sita tu, huku katika michuano ya CAF, akiisaidia timu hiyo kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiongoza msimamo wa Kundi A kwa kukusanya pointi 13 na kufunga mabao manane na kufungwa manne tu.

Idadi ya mabao hayo manne imeifanya Simba kuwa ni timu iliyoruhusu mabao machache katika kundi hili lililokuwa na CR Belouizdad wa Algeria, Bravos do Maquis ya Angola na Sfaxien ya Tunisia.

Mbali na kutengeneza ukuta mgumu, Che Malone pia ni mmoja ya wachezaji walioifungia Simba mabao katika Ligi Kuu akiwa na mawili kati ya 38 iliyonayo timu hiyo itkayoshuka uwanjani kesho Jumatano kuvaana na Namungo ikiwa ugenini Ruangwa, mkoani Lindi.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alizungumzia mchango wa beki huyo akisema: “Che Malone ni mchezaji wa kipekee. Yeye ni beki ambaye ni nguzo muhimu katika ulinzi wetu, na tunaendelea kuhitaji mchango wake. Anaweza kupambana na washambuliaji wa timu pinzani kwa ustadi na ana nguvu ya kuongoza safu ya ulinzi.”

Kwa upande wa Che Malone aliwahi kukaririwa akisema: “Simba ni familia yangu, na ni furaha kufanya kazi na timu hii. Kila siku ni nafasi ya kujituma zaidi na kusaidia timu kufikia malengo yake.”

Simba itashuka kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa kuivaa Namungo ikiwa ni mechi ya 19 kwa timu hiyo baada ya mchezo uliokuwa upigwe wikiendi iliyopita dhidi ya Dodoma Jiji kuahirishwa baada ya wapinzani wao kupata ajali ikitokea Lindi ilipoenda kuicheza na Namungo na kutoka sare ya 2-2.

SOMA NA HII  ISHU YA MAYELE KUBAKI AU KUONDOKA UONGOZI WA YANGA WATOA NENO HILI