Home Habari za michezo BOYELI NA JANGWANI KWISHA HABARI

BOYELI NA JANGWANI KWISHA HABARI

37
0

UONGOZI wa Klabu ya Yanga umetangaza rasmi kuachana na aliyekuwa nyota wao, Andy Boyeli, baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa mkopo wa miezi sita aliokuwa akiitumikia timu hiyo.

Taarifa hiyo imetolewa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, ambaye amesema pande zote mbili zimefikia makubaliano ya kumalizana kwa amani.

Boyeli alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu akitokea klabu ya Sekhukhune United ya Afrika Kusini kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita.

Licha ya kupewa nafasi katika kikosi, mshambuliaji huyo hakufanikiwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa na benchi la ufundi pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Yanga uliona ni busara kutomwongezea mkataba baada ya muda wake wa mkopo kukamilika, kuruhusu arejee katika klabu yake ya Sekhukhune United.

Kamwe amesema uamuzi huo umezingatia tathmini ya kiufundi pamoja na mipango ya baadaye ya timu.

Ameongeza kuwa Boyeli ni miongoni mwa wachezaji wachache waliopata baraka ya kuondoka rasmi katika dirisha la usajili, hadi sasa hakuna mchezaji mwingine aliyeachwa zaidi ya waliotangazwa wazi.

Mbali na Boyeli, Kamwe amethibitisha pia kuondoka kwa mchezaji mwingine, Denis Nkane, ambaye amepelekwa kwa mkopo kujiunga na timu ya TRA kwa ajili ya kupata nafasi zaidi ya kucheza na kuendeleza kiwango chake.

Kwa mujibu wa Kamwe, Yanga itaendelea kufanya maamuzi ya kimkakati kuhusu kikosi chake ili kuhakikisha timu inakuwa imara zaidi katika mashindano mbalimbali yanayoendelea, huku ikizingatia maslahi ya klabu na maendeleo ya wachezaji wake.