Mashujaa FC
Michezo Bongo

Kocha Josiah Aifungia Kazi Mashujaa FC Kuelekea Dhidi ya Kagera Sugar

Vardo August 25, 2026 8:12 pm

BAADA ya kukamilisha safari ya dakika 270 ugenini na kuondoka na pointi tatu pekee, Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Aman Josiah, amefungia kazi kikosi chake kuelekea mchezo wao unaofuata wa Ligi Kuu ya NBC nyumbani mkoani Kigoma.

Mashujaa ilianza mzunguko wake wa ugenini kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, kabla ya kupokea vipigo viwili mfululizo kutoka kwa Fountain Gate (1-0) na Mbeya City (2-1). Sasa timu hiyo inarejea katika Uwanja wa Lake Tanganyika kujiandaa na mpambano dhidi ya Kagera Sugar.

Akizungumzia mwenendo huo, Kocha Josiah alikiri ugumu wa ligi na uchovu wa safari, lakini akasisitiza kuwa hakuna sababu ya kutojipanga upya ili kupata matokeo mazuri na kurejesha morali ya timu.

“Kwa sasa hatuna namna zaidi ya kujipanga na mechi ijayo nyumbani dhidi ya Kagera Sugar. Lazima tukubali ugumu wa ligi na namna ya kukabiliana nao, vijana wanao uwezo wa kubadili matokeo. Pointi tatu ugenini si mbaya sana japo si matokeo bora kwa timu yenye malengo makubwa,” alisema Josiah.

Kocha huyo aliongeza kuwa katika mchezo dhidi ya Mbeya City, saikolojia ya wachezaji ilionekana kushuka, hivyo benchi la ufundi linakwenda kusahihisha makosa na kurekebisha mbinu ili kurejesha kasi yao.

Kwa upande wake, beki na nyota wa timu hiyo, Hija Shamte, alibainisha kuwa kila mchezo mbele yao ni vita ya kusaka pointi tatu.

“Matarajio yetu ni kuona Mashujaa inafanya vizuri kwa sababu kila mchezaji ana kiu ya mafanikio. Matokeo ya mechi zilizopita si mazuri sana, hivyo lazima tupambane kufikia malengo yetu,” alisema Shamte.

Simba SC Yaweka Wazi Vita ya Ligi ya Mabingwa Afrika: “Lengo Letu Ni Nusu Fainali” Michael Carrick Matatani Man United: Eddie Howe Kutajwa Kuchukua Mikoba