Sakata La Mastaa Yanga Stars Lafukuta, TFF Yajibu Taarifa Za Gamondi Kuchukizwa
Sakata la wachezaji wa Yanga kuruhusiwa kuondoka kambini Taifa Stars nchini Morocco limezua mjadala mkubwa, huku jina la kocha Miguel Gamondi likivutwa katikati baada ya taarifa kusambaa kwamba hakuridhishwa na uamuzi huo.
Nyota wanne wa Yanga waliotajwa kuruhusiwa kurejea Dar es Salaam ni Mudathir Yahya, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Seleman Mwalimu na Mohamed Hussein. Sababu kubwa inayotajwa ni kuwahi kujiunga na maandalizi ya klabu yao kuelekea Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba.
Hapo ndipo maswali yakaanza. Kwa nini Yanga? Je, Gamondi alikuwa amekubali? Na Stars ambayo bado ina ratiba Morocco inaachaje wachezaji muhimu waondoke?
TFF Yavunja Ukimya
Katibu Mkuu wa TFF, Evance Mgeusa, amesema Yanga haikupewa upendeleo wa kipekee. Kwa mujibu wake, Simba na Singida pia ziliomba baadhi ya wachezaji wake waliopo Taifa Stars waruhusiwe kurejea klabuni na maombi hayo yakakubaliwa.
Mgeusa pia amesema benchi la ufundi la Stars lilishirikishwa kabla ya uamuzi huo kufanyika na Gamondi alitoa baraka zake. Hivyo TFF imekanusha taarifa zilizokuwa zinasambaa kwamba kocha huyo alichukizwa na wachezaji kuondoka kambini bila utaratibu.
Lakini Maswali Bado Yapo
Hata kama TFF imeweka msimamo wake wazi, timing ya uamuzi ndiyo inayofanya mjadala huu usife haraka. Taifa Stars bado iko Morocco, ina mechi za majaribio na Gamondi yuko kwenye kipindi cha kujenga kikosi kuelekea AFCON 2027.
Wakati huo huo Simba na Yanga zina Dabi Oktoba 10, mchezo ambao klabu zote mbili zinataka kuingia zikiwa na wachezaji wake wote na muda wa kutosha wa maandalizi. Hapo maslahi ya timu ya taifa na klabu yanakutana uso kwa uso.
Yanga Inawahitaji Sana
Kwa Manqoba Mngqithi, kurejea mapema kwa Bacca, Mudathir, Mohamed Hussein na wengine ni faida kubwa. Yanga imekuwa ikifanya maandalizi ikiwa na kundi pungufu kutokana na wachezaji wengi kuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa.
Kadri hao wanavyorudi, ndivyo kocha anavyopata nafasi ya kuanza kuweka pamoja starting XI na tactical plan yake ya Dabi. Simba na Yanga zote zimeanza msimu vizuri, hivyo kila siku ya maandalizi ina thamani kubwa.
Stars Nayo Ina Sababu Zake
Baada ya kupoteza 5-0 dhidi ya AS FAR, upande wa Taifa Stars nao una hoja nzito. Hii ndiyo kipindi ambacho kocha angependa kuwa na wachezaji wake wote ili kufanya marekebisho ya haraka na kupata reaction kabla ya mchezo unaofuata.
Ndiyo maana hata kama TFF imesema kila kitu kilifanyika kwa makubaliano, mjadala huu utaendelea kwa sababu kila upande una sababu ya kutaka wachezaji hao.
Soma Hapa: Yanga Yaingia Kwenye Hesabu Za Dabi Bila Mastaa 15, Manqoba Ana Kazi