KOCHA wa Azam FC Idd Cheche amesema kuwa haikuwa bahati mbaya wao kutwaa ubingwa wa kombe la Shirikisho mbele ya Lipuli mchezo uliochezwa uwanja wa Ilulu, Lindi kwa kuwa walijipanga mapema na walitambua aina ya timu waliyokutana nayo.
Azam FC watapeperusha Bendera ya Tanzania kimataifa baada ya kutwaa kombe la FA kwa mara ya kwanza baada ya kushinda bao 1-0 lililopachikwa kimiani na mshambuliaji Obrey Chirwa dakika ya 64.
Akizungumza na Salehe Jembe, Cheche amesema kuwa umakini wa wachezaji pamoja na michezo migumu ya mwisho kwenye ligi kuu iliwafanya wawe bora na kutengeneza kikosi imara ambacho kimewapa matokeo.
“Utayari wa wachezaji na kufuata kile ambacho wameelekezwa kumefanya iwe rahisi kwetu kuibuka na ushindi hivyo ni muda wetu kupeperusha bendera kimataifa, hesabu zetu zimekamilika tunawashukuru mashabiki kwa sapoti yao.
“Kwenye mchezo ni lazima kuwe na mbinu ili kushinda, tulianza kukiaanda kikosi mapema hasa baada ya kupoteza nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu, tulitambua aina ya timu tunayokutana nayo ni ngumu hivyo nasi tulifanya maandalizi magumu kuwakabili mwisho wa siku tumefanikiwa,” amesema Cheche.