Home Uncategorized AZAM YABEBA UBINGWA WA FA, YAICHAPA LIPULI 1-0 KWA MBINDE

AZAM YABEBA UBINGWA WA FA, YAICHAPA LIPULI 1-0 KWA MBINDE


Azam FC imeandika rekodi ya kutwaa taji la Kombe la Shirikisho ‘Azam Sports Federation CUP’ kwa mara ya kwanza kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lipuli FC katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.

Bao pekee la Obrey Chirwa mnamo dakika ya 64 ya kipindi cha pili limeipa Azam matokeo hayo na kuiwezesha kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Kunako kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa ari ya kusaka mabao ya mapema lakini uimara wa safu zote mbili kwenye ulinzi ulizuia nyavu kuguswa.

Timu zote zilionesha kushambuliana kwa zamu kwa takribani dakika zote 90 huku safu za ulinzi zikifanya kazi yake maradadufu kiasi ambacho kilipelekea kusiwepo na wingi wa mabao.

Mechi hiyo ambayo imekuwa ya kwanza kwa fanali ya FA kupigwa kupigwa mkoani Lindi, imeshuhudiwa na watazamaji wengi ambao walijitokeza kwenye Uwanja wa Ilulu, na hii ni kutokana na ugeni wa timu hizo mbili mjini humo.

Ushindi huu unaifanya Azam kutinga kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza kupitia mashindano haya ya ASFC.

Aidha, Azam wameingia fainali kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwa michuano hii baada ya kupoteza msimu wa 2015/16 dhidi ya Yanga kwa mabao 3-1, mechi ikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ikumbukwe Lipuli walifanikiwa kutinga hatua ya fainali kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga huko Samora Stadium mjini Iringa na Azam wakiifunga KMC bao 1-0, mechi ikichezwa Chamanzi Complex.

Ukiachana na Azam kuwa bingwa hii leo, taji hilo lilichukuliwa na Mtibwa Sugar msimu uliopita ambayo ilitwaa kwa kucharaza Singida United kwa jumla ya mabao 3-2, mechi ikichezwa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Na George Mganga

SOMA NA HII  WILLIAN ANAAMINI ARSENAL ITATWAA UBINGWA WA LIGI KUU ENGLAND