Home Uncategorized VIFAA VIWILI VYASAINI YANGA

VIFAA VIWILI VYASAINI YANGA


YANGA bado wako bize kwelikweli na mambo ya usajili ambapo juzi usiku walikamilisha usajili wa mastaa wawili ambao wanaaminika watabadili mambo na kuirejesha ile Yanga ya kimataifa msimu ujao.

Klabu hiyo yenye makazi yake mitaa yenye kelele kibao pale Jangwani jijini Dar iko bize kusajili wachezaji ambao walipendekezwa na kocha wao, Mwinyi Zahera ambaye kwa sasa yuko Hispania kwenye kambi ya DR Congo inayojiandaa na mashindano ya Afcon.

Mpaka sasa Yanga imekamilisha usajili wa mastaa kama Erick Rutanga kutoka Rayon Sports ya Rwanda, Lamine Moro (Buildcon, Zambia), Issa Bigirimana ‘Walcott’ (APR, Rwanda), Maybin Kalengo (Zesco, Zambia). Wengine ni Abdul Aziz Makame (Mafunzo FC, Zanzibar) na Ally Mtoni Sonso (Lipuli FC, Iringa).

Sasa usiku wa kuamkia jana, timu hiyo imeingia makubaliano na kumsaini kipa wa Bandari FC ya Kenya, Farouk Shikalo na mshambuliaji chipukizi wa Zesco, Maybin Kalengo mwenye umri wa miaka 20.

Wachezaji hao wamekamilisha idadi ya wachezaji sita kutoka nje ya nchi na watatu wazawa ambao tayari wamesaini mikataba ya kuvaa jezi zenye rangi ya kijani, njano na nyeusi katika msimu ujao.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumamosi imezipata, wachezaji hao wote juzi usiku rasmi walisaini mikataba ya miaka miwili ya kuichezea Yanga ya Mshindo Msolla ambaye ndiye kiongozi msomi zaidi kwenye Ligi Kuu Bara akiwa na falsafa ya Udaktari.

Chanzo chetu cha habari kilipasha kwamba Shikalo baada ya kusaini mkataba huo haraka jana asubuhi alipanda ndege na kurejea Kenya kwa ajili ya kujiunga na timu ya Taifa inayojiandaa na Afcon. Kenya iko kundi C na Taifa Stars.

“Kati ya hao yupo kipa mmoja kutoka Bandari ya Kenya ambaye Shikalo yeye alisaini na kurejea nyumbani kwao Kenya kwa ajili ya kujiunga na timu ya Taifa ya Kenya, pia Kalengo alisaini mkataba katika kuisuka safu ya ushambuliaji,” kilisema chanzo chetu cha kuaminika.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alizungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Bado tunaendelea kukisuka kikosi chetu kwa kusajili wachezaji wote ambao kocha alitoa mapendekezo yake katika usajili, hivyo ni kweli tumefikia makubaliano mazuri na kusaini mikataba.” Naye Shikalo baada ya kusaini alizungumza na Championi na kusema:

“Nimesaini mkataba wa miaka miwili Yanga, licha ya kuwepo kwa baadhi ya vipengele ambavyo tulikubaliana na viongozi ambavyo nitavimaliza baada ya kutoka Afcon kwa sababu leo (jana) timu inakwenda Ufaransa kwenye kambi ya maandalizi.”

Wakati huohuo, kipa Metacha Mnata kutoka Mbao FC, anatarajiwa kusaini mkataba wa kuichezea yanga leo Jumamosi asubuhi kabla ya kujiunga na kambi ya Taifa Stars.

SOMA NA HII  AZAM FC WATAKA KUCHEZA MECHI MBILI TU KAGAME