Home Uncategorized BALINYA AMTIKISA KAGERE BONGO

BALINYA AMTIKISA KAGERE BONGO


MSHAMBULIAJI mpya wa kikosi cha Yanga, Juma Balinya aliyesajiliwa na klabu hiyo kutoka Polisi ya Uganda, amefunguka kuwa moja ya malengo yake kwa msimu ujao ni kuhakikisha anarudia kitendo alichokifanya nchini
kwao cha kuwa mfungaji bora.

Balinya ni miongoni mwa nyota 10 wapya wa kikosi cha Yanga ambao wamesajiliwa kwa ajili ya msimu ujao.

Mshambuliaji huyo msimu uliomalizika katika Ligi Kuu ya Uganda, aliibuka mfungaji bora baada ya kupachika mabao 19 ambapo kauli yake hiyo ni kama kumtangazia vita, Meddie Kagere wa Simba ambaye msimu uliomalizika mwezi uliopita, alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa kufunga mabao 23.

Balinya amesema kwamba anajua majukumu yake ni kufunga hivyo ataongeza
nguvu kuhakikisha anafunga mabao mengi ili amalize na mabao mengi katika ligi.

“Najua majukumu yangu ni kufunga, hivyo nitakapokuja malengo yangu ni kufunga zaidi, niwe namba moja katika timu lakini kwenye ligi kwa ujumla.

“Najua nitakutana na changamoto mpya kwa sababu ndiyo mara ya kwanza kucheza huko, lakini niseme nishazoea kwa ajili ya kupambana hivyo halitakuwa jambo gumu kwangu kutimiza hicho ambacho mimi nimejipangia,” alisema Balinya. Hali hii inaonyesha kuwa msimu ujao kutakuwa na ushindani mkubwa kwenye ligi katika safu ya ufungaji bora.

SOMA NA HII  JAMBO LISIWE GUMU MASTAA SIMBA WAJAZWA MINOTI MAPEMA AFL DHIDI YA AL AHLY