Home Uncategorized KAPOMBE ABEBA MILIONI 70 SIMBA

KAPOMBE ABEBA MILIONI 70 SIMBA


Imefahamika kuwa beki kiraka wa Simba, Shomari Kapombe amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kukipiga Msimbazi kwa dau la Shilingi Milioni 70.

Kapombe ni kati ya wachezaji sita walioongezewa mikataba yao hivi karibuni baada ya kumalizika wengine ni John Bocco, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Meddie Kagere na Clatous Chama.

Simba, pia imewasajili wachezaji wapya ambao ni Sharaf Eldin Shiboub, Ali Abdalrahman, Wilker Henrique da Silva, Gerson Fraga Vieira, Beno Kakolanya na Kennedy Juma.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Simba, ni kuwa beki huyo amesajiliwa kwa kiasi hicho cha fedha baada ya kufikia muafaka mzuri katika dau la usajili ambalo amelihitaji.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, awali beki huyo alikuwa akihitaji Shilingi Milioni 80 kabla ya kuzungumza na viongozi na kukubali kusaini kwa dau hilo la fedha.

“Kapombe siyo mchezaji mbaya ni mzuri ana kiwango kizuri na majeraha siyo kikwazo cha yeye kumuongezea mkataba mwingine mpya wa kuichezea Simba.

“Kapombe ameongezea mkataba huo baada ya kukubaliana baadhi ya vitu ikiwemo mshahara na dau la usajili ambalo hilo amelitaka yeye.

“Awali, kulikuwepo na mvutano kati yake Kapombe na viongozi wa Simba katika dau la usajili kati ya lake alilokuwa analitaka yeye na la uongozi ambalo walimuwekea mezani Shilingi Milioni 70,” alisema mtoa taraifa huyo.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi kuzungumzia hilo alisema kuwa “Mkataba wa mchezaji ni siri kati ya viongozi na mchezaji husika, hivyo sitaweza kuweka wazi dau hilo la usajili.”

SOMA NA HII  POGBA: SIPENDI KUONA LIVERPOOL IKITWAA UBINGWA, TULISTAHILI SISI KUUBEBA