Home Uncategorized KIPI HASA KINAKUUMIZA KWA AJIBU NA JONAS MKUDE?

KIPI HASA KINAKUUMIZA KWA AJIBU NA JONAS MKUDE?

Na Saleh Ally
MIAKA mitatu iliyopita wakati kikosi cha Taifa Stars kambini nchini Uturuki, Kocha Mkuu Charles Boniface Mkwasa alilalamika kuhusiana na wachezaji wavivu wa mazoezi. Kati ya aliowataja alikuwa ni Ibrahim Ajibu na Abdi Banda.
Mkwasa alimueleza Banda mbele yetu tuliokuwa mazoezini katika kambi katika Mji wa Kartepe, Uturuki kwamba kama atamuita tena akaumia wakati wa mazoezi ya kupima utimamu wa mwili, basi hatamuita tena kwa kuwa kuumia kwenye mazoezi hayo ya mwanzo ya kambi ni ishara tosha ya uvivu.
Tukiwa Uturuki nilipata bahati ya kuzungumza na Banda ambaye alilalamika kiasi fulani lakini kuna ambayo alikubaliana nayo. Kuanzia hapo, nikawa na ukaribu na Banda kama mdogo wangu tukikumbushana masuala kadhaa.
Banda alibadilika na huenda kati ya wachezaji wanaoaminika ni makini na kazi, wanaopenda na kutimiza haki ya mazoezi ni Banda. Wakati nikiwa Afrika Kusini kumfanyia mahojiano, nilibahatika kuzungumza na kocha wake, Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi la Baroka FC, Dokta Khumalo ambao wote walimsifia na kunieleza kumteua kuwa mmoja wa manahodha wa timu hiyo.
Wakati Banda akiwa amebadilika, mara zote tumesikia kuhusiana na suala la uvivu wa mazoezi wa wachezaji kadhaa nyota mfano Ajibu, Jonas Mkude na wengine. Kila mmoja anakubaliana na kipaji walichonacho lakini tatizo kubwa limekuwa ni suala la uvivu au nidhamu.
Kawaida, unapokuwa mvivu wa mazoezi, maana yake huna nidhamu. Kama utekelezaji wako wa mazoezi utakuwa wa kiwango cha chini, maana yake husikilizi kile ambacho unaelezwa na kocha au makocha wengine.
Nidhamu ya chini imewaangusha sana wachezaji wengi nchini ambao baadhi yao wamekuwa kipenzi cha mashabiki wa soka ambao hawajui undani wa wachezaji hao.
Jana, Kocha Mkuu wa Taifa Stars ametangaza kikosi cha wachezaji walioondoka kwenda Cairo kwa ajili ya kambi akiwa amewatema wachezaji saba wakiwemo Ajibu na Mkude ambao wamezua gumzo kubwa.
Ajibu amecheza Simba na Yanga, Mkude amekuwa Simba tu na wote wamekuwa vipenzi vya mashabiki wa timu hizo mbili na hasa Simba kwa kuwa ni vijana waliokulia katika timu yao ya vijana.
Hakuna ubishi, Ajibu na Mkude wamekuwa kati ya wachezaji wanaozungumzwa katika masuala ya nidhamu na mara kadhaa wamekuwa wakiingia katika msigano na baadhi ya makocha na sote tunalijua hili.
Mkude na Ajibu wana vipaji, lakini adui mkubwa wa vipaji vyao ni ukosefu wa juhudi sahihi, nidhamu ya kutosha kuwafanya waviendeshe vipaji vyao. Ni sawa na kusema gari yenye uwezo wa kubeba tani 10 lakini matairi yake ni yale yenye uwezo wa tani tatu hadi tano.
Kuna tatizo kubwa kwa Ajibu na Mkude na wengine wa aina yao. Tumesikia matatizo mengi sana lakini ushabiki umewafunga macho wadau wengi wa soka, wameendelea kuwaunga mkono wachezaji hao kwa kuwa wana uwezo wa kutoa pasi nyingi za mabao au kupiga pasi wanapokuwa uwanjani.
Ushabiki umewafanya wachezaji waendelee kuwa na hisia za kifalme, ambazo zinawainua kwa maana ya hisia lakini uhalisia unawaangusha. Kila wanachoambiwa si sahihi, wanaona wanaonewa kwa kuwa jamii inayowazunguka imekuwa na unafiki badala ya urafiki kwao.
Unafiki kwa kuwa wanaowatetea wanajali furaha wanayoipata kutoka kwa wachezaji hao kutokana na ushabiki lakini uhalisia ni kweli hawako sahihi na lazima wajipime kwa kuwa haiwezekani makocha wazalendo, wageni wote wawe wanawaona wachezaji hao wana tatizo.
Katika maendeleo ya mpira, umahiri kutokana na kipaji pekee haumfanyi mchezaji kuwa bora zaidi. Sote tunajua kuhusiana na kipaji cha Mbwana Samatta lakini sote tunafahamu ubora wa nidhamu yake ambayo kwa jumla, leo anakuwa mfano namba moja wa kuigwa.
Sote tunajua, kwa asilimia kubwa Ajibu anaweza kuwa na kipaji cha juu hata kuliko Simon Msuva, lakini angalia hatua na maendeleo ya Msuva na Ajibu, ni mbingu na ardhi na bahati mbaya wenye mapenzi na wachezaji hao tunashindwa kuwasaidia kwa visingizio tofauti lakini kikuu ni madai kuwa wanaonewa.
Ajibu na Mkude, pia wengine wenye tabia kama zao lazima wajipange na kubadilika kwa kuwa dunia imebadilika kwa kuwa wachezaji wasio na vipaji vya kutisha, wamekuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na kiwango kikubwa cha nidhamu wanachokuwa nacho.
Wachezaji wenye vipaji ndiyo wamekuwa wakihangaika, wakipata nafasi ya kutamba kwa muda mfupi sana kwa kuwa nidhamu ni msingi mkuu wa maendeleo na mafanikio kwa wachezaji na si kipaji pekee.
Endeleeni kuwatetea Ajibu na Mkude, wao pia wandelee kufanya wanachoamini ni sahihi licha ya kwamba ni sahihi, mwisho wake wataendelea kushuhudia wale ambao wanaamini ni wa kawaida wakisonga mbele na kucheza Ulaya kwingineko kwenye mafanikio zaidi.
Angalia, leo Ajibu anabaki lakini Miraji Athuman wa Lipuli FC anakwenda Afcon, tafakari hili au Mkude anabaki halafu Mudathir Yahaya, kinda zaidi kwake au Fred Tangalu wa Lipuli FC wanakwenda Afcon.
Unaweza kuchukulia kawaida lakini kwa uhalisia katika hili, mpongezeni Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike kwa kuwa uchaguzi wake unaonyesha umeangalia vigezo sahihi badala ya majina tu, kama ambavyo kocha wa Simba anaweza akasumbuliwa na Mkude lakini akaamua kukaa kimya kwa hofu ya mashabiki au baadhi ya viongozi wanaompenda Mkude.
Kuna kitu cha kujifunza na Mkude na Ajibu kwa walipofikia, si jambo sahihi wao kushindwa kwenda Afcon.
Lakini aliyewafanya washindwe kwenda ni wao wenyewe na wadau tukitaka tuwe sehemu ya kusaidia, basi tunapaswa kuwa wakweli kwao badala ya kuishi nao kinafiki tukiwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa mwisho wao ndiyo unakuwa huu wa kuishia Dar es Salaam na Cairo kuishuhudia runingani. 

SOMA NA HII  JKT TANZANIA YASIMAMISHA USAJILI WA KMC