Jana tarehe 12 June kilifanyika kikao cha Bodi ya Simba Sports Club Company Limited. Kikao hiki kilifikia maazimio mbali mbali juu ya maendeleo ya Klabu yetu.
1.0 Taarifa juu ya maendeleo ya mabadiliko ya muundo wa Klabu kuwa kampuni ( Transformation)
Itakumbukwa kuwa Klabu ilijipa muda wa mpito ( transition) wa kukamilisha ubadilishaji wa muundo wa mabadiliko ya Klabu kuwa Kampuni. Bodi imeridhika na hatua iliyofikiwa ya ukamilishaji wa muundo wa Kampuni na imeongeza nguvu kazi ya ukamilishaji wa muundo wa Kampuni. Bodi imewateua Aziz Kefile, Mulamu Ng’ambi, Barbara Gonzalez, na Wanasheria wa Kampuni ya Simba Evodius Mtawala na Michael Mhina kukamilisha kwa haraka hatua ndogo iliyobaki. Ni matarajio ya Bodi kuwa ndani ya miezi miwili kila kitu kitakuwa kimekamilika.
2.0 Bunju Project
Bodi imepokea taarifa ya maendeleo ya sehemu ya mazoezi ya Klabu ya Simba iliyoko Bunju ( Training centre). Baada ya mvua kumalizika matengenezo ya kuandaa uwanja kwa ajili ya kuweka nyasi bandia yataendela, sambamba na ujenzi wa vyumba vya kubadilishia nguo ( changing rooms), na uwanja wa nyasi za kawaida.
Sambamba na hilo Bodi imemteua aliyekuwa Meneja wa zamani wa Simba Richard kuwa Msimamizi wa Mradi wa maendeleo wa Bunju.
3.0 Kandarasi ya jezi za msimu wa 2019/20
Bodi imepitisha mapendekezo ya kamati ndogo ya Bodi iliyoundwa kutafuta Mzabuni wa jezi za Simba kwa msimu ujao wa Ligi. Baada ya ushindani wa Makampuni matatu Novum Pharm ( Starbalm), Umbro na UHL ( Romario), Kampuni ya UHL Romario imeshinda Zabuni hiyo. Mkataba utasainiwa hivi karibuni na baadaye uzinduzi wa jezi mpya ya msimu ujao utafanyika.
Simba week ya Mwaka huu 2019 itaanza tarehe 1/8/2019 kwa kushirikisha WanaSimba na Watanzania wote nchi nzima. Mchezo wa kuhitimisha Simba week ambayo ndiyo itakuwa kilele cha Simba week maarufu kama Simba Day itakuwa tarehe 8/8/2019. Timu ambayo imealikwa mtajulishwa ijumaa hii. Bodi pia imeteua kamati ndogo ya Simba Week kufanya kazi kwa niaba yake.
Usajili kwa Wachezaji wa ndani umekamilika kwa asilimia 90. Sasa mashambulizi yameanza kwa Wachezaji wa nje ya nchi. Taarifa za Wachezaji waliosajiliwa zitakuwa zinatolewa kila leo kupitia kurasa za Mitandao ya Simba kila leo.
.
Bodi imepitisha mpango wa uzinduzi wa kadi mpya za Wanachama na Wapenzi wa Simba. Uzinduzi huu unatarajiwa kufanyika ndani ya siku 10 kuanzia leo.