Home Uncategorized WATANO WASAINI RASMI YANGA

WATANO WASAINI RASMI YANGA


Uongozi wa Yanga ulikuwa kwenye hatua ya kuwasainisha mikataba mipya nyota wake watano tayari kwa kuwatumia msimu ujao kwenye michuano mbalimbali. Timu hiyo inaanza kambi rasmi ya mazoezi Jumapili ijayo mjini Morogoro.

Yanga imeendelea kufanya usajili huo ikiwa ni siku chache tangu wakamilishe usajili wa wachezaji wake wanne, Gadiel Michael, Metacha Mnata, Ally Mtoni Sonso na kipa wa timu ya Taifa ya Kenya, Farouk Shikhalo ambao wote wapo Misri kwenye Kombe la Afrika ‘Afcon’.

Tofauti na wachezaji, wengine waliosajiliwa na Yanga ni Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama, Ally Ally, Issa Bigirimana ‘Walcott’, Patrick Sibomana, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo, Juma Balinya, Lamine Moro na Suleyman Mustapha.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, wachezaji waliotarajiwa kusaini mikataba hiyo jana usiku ni Mrisho Ngassa, Raphael Daudi, Juma Mahadhi, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Deus Kaseke.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, mastaa hao wanasaini mikataba hiyo baada ya kufikia muafaka mzuri na wachezaji hao wote katika dau la usajili wanalolitaka na mshahara wa kila mwezi.

“Uongozi umefanya mawasiliano na kocha Zahera (Mwinyi) juu ya wachezaji anaowahitaji kuwabakisha kwa wale ambao mikataba yao imemalizika mwishoni mwa msimu huu.

“Majina hayo tumeyapanga kuyatangaza siku yoyote kuanzia hivi sasa, lakini kwa wachezaji ambao amependekeza waongezewe mikataba ni Ngassa, Kaseke, Raphael, Ninja na Mahadhi.

“Wachezaji hao walitarajiwa kusaini mkataba jana (juzi) lakini kutokana na ratiba kubana tukasogeza mbele na hivyo watasaini leo (jana) usiku,” alisema mtoa taarifa huyo.

Championi lilimtafuta mmoja wa wachezaji hao, Ngassa atoe neno kuhusiana na ishu hiyo ambapo alisema: “Ni kweli ilikuwa nisaini mkataba jana (juzi) lakini ikashindikana na sasa ninasaini leo (jana) usiku baada ya makubaliano mazuri ya pande zote.”

Naye Mwenyekiti wa Yanga, Dr Mshindo Msolla hivi karibuni alisema kuwa: “Kwa asilimia 70 tayari tumekamilisha usajili wa wachezaji tunaowahitaji kwa ajili ya msimu ujao. “Wapo wapya na wale tutakaowaongezea mikataba baada ya kufikia muafaka mzuri na kukubali kusaini kubaki Yanga na usajili huo tumeufanya kwa mujibu wa mapendekezo ya kocha wetu.”

WALIOPEWA MKONO WA KWAHERI HAWA HAPA

Yanga tayari imeshawapa barua wachezaji wao nane ambao wameachana nao hivyo msimu ujao wachague kwa kwenda. Wachezaji hao ni, Yusuf Mhilu, Said Juma Makapu, Jafary Mohammed, Klaus Kindoki, Ibrahim Ajibu, Amissi Tambwe na Thaban Kamusoko.

SOMA NA HII  MFUMO MPYA WA BONASI NDANI YA YANGA WABADILIKA