Home Uncategorized NINJA ALIPWA MSHAHARA WA BILIONI 2 MAREKANI, ATACHEZA NA ZLATAN LA GALAXY

NINJA ALIPWA MSHAHARA WA BILIONI 2 MAREKANI, ATACHEZA NA ZLATAN LA GALAXY


IMEFAHAMIKA kuwa beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye kwa sasa anakwenda LA Galaxy ya Marekani kwa mkopo, atakuwa akilipwa mshahara wa euro 18,000 (Sh milioni 46.7) kwa wiki, ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 2.2 kwa mwaka.

Ninja ambaye amesaini mkataba wa miaka minne katika Klabu ya MFK Vyškov ya Jamhuri ya Czech, anapelekwa Marekani kucheza kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Ninja aliyeitumikia Yanga kwa misimu miwili mfululizo akitokea katika Klabu ya Taifa Jang’ombe ya Zanzibar, ameamua kutafuta changamoto mpya nje ya nchi, baada ya mkataba wake na klabu hiyo kumalizika mwishoni mwa msimu huu huku akidaiwa kulamba mshahara wa zaidi ya euro elfu 18 kwa wiki ambayo ni zaidi ya Sh milioni 46.7 za Kitanzania.

Chanzo makini cha habari hii kimelinyetishia Championi Jumatano kuwa, Kampuni ya Dream World Sport, imemwezesha kuingia mkataba huo, ambao utamfanya
kulipwa kwa kila wiki kiasi hicho.

Kwa malipo hayo, maana yake ni kuwa kwa mwezi atakuwa anakusanya zaidi ya shilingi milioni 187 na kwa mwaka mmoja ni shilingi bilioni 2.2, hii ni kabla ya kukatwa kodi zote stahiki za nchi husika.

“Tunawapongeza sana Kampuni ya Dream World Sport kwa kumwezesha kijana wetu Ninja kupata klabu nje na kubwa kama hiyo, ni jambo la kujivunia sana, hivyo tunamtakia kila la heri katika majukumu yake mapya kwani uzoefu atakaoupata huku utakuwa msaada mkubwa kwa taifa letu.

“Ninja ameondoka Yanga vizuri, hivyo hatuna budi kumtakia la heri, zaidi tumuombee aweze kufanya vyema kwani mafanikio yake ni sifa kwa Yanga ambayo ndiyo timu yake ya mwisho kuitumikia, hivyo imani yetu ataendelea kuitangaza siku zote za maisha yake ya soka,” kilisema chanzo hicho.

LA Galaxy ni timu kubwa inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani na Canada (MLS) ambayo wamewahi kuichezea mastaa kibao akiwemo David Beckham, ambayo pia hivi sasa anakipiga staa wa zamani wa Barcelona na PSG, Zlatan Ibrahimovic

SOMA NA HII  MORRISON: NILICHEZA MECHI MBILI BILA KUWA NA MKATABA NDANI YA YANGA