Home Uncategorized TUNAHITAJI AKINA AZAM FC, KMC KIBAO ILI KUIBADILISHA TANZANIA

TUNAHITAJI AKINA AZAM FC, KMC KIBAO ILI KUIBADILISHA TANZANIA

NA SALEH ALLY
KATI ya timu za Tanzania zinazokwenda katika michuano ya Kombe la Kagame ni Azam FC ambao ni mabingwa watetezi pamoja na KMC ya Kinondoni jijini Dar.

Michuano hiyo itashirikisha timu za mataifa mbalimbali kama DR Congo, wenyeji Rwanda pamoja na Kenya, Uganda na nyinginezo.

Hii ni michuano ya kimataifa ambayo ingekuwa na faida kubwa kwa ukanda dhaifu wa Afrika Mashariki unapozungumzia ubora wa soka. Lakini imekuwa haina faida kutokana na uongozi mbovu na wa kusuasua wa Baraza la Vyama vya Soka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Katibu wake, Nicholas Musonye amekuwa kama mfalme, ameendelea kubaki hapohapo kama mfalme na umeona baada ya Simba na Yanga kujiondoa, amekuwa akivurumisha maneno ya mipasho badala ya kusikiliza hoja zao na kuzijibu kwa utaratibu mzuri.

Tuachane na Musonye kwa kuwa nilichokilenga zaidi ni faida ya kuwa na timu mpya za Tanzania katika michuano hiyo.

Kama Simba na Yanga zingeenda, maana yake KMC isingekuwa na nafasi ya kushiriki. Azam FC wao wangeenda kama mabingwa watetezi.

Ukiangalia kwa undani utagundua Azam FC wamefaidika sana na michuano hii ya Kagame kuwakuza na kuwasaidia kuwa imara zaidi.

Wamekuwa imara zaidi kwa kuwa walipata nafasi ya kukutana na timu kutoka katika mataifa mbalimbali na si Tanzania pekee.

Msaada huo uliwafanya kuwa imara zaidi na unaona wamefanikiwa kubeba ubingwa zaidi ya mara moja, jambo linaloonyesha kweli kuna msaada.

Safari hii ukiachana na timu za Zanzibar ambazo mara nyingi hazijafanikiwa katika michuano hii, KMC wanakwenda kwa mgongo wa Simba na Yanga zilizogoma kwenda lakini wanaweza kuwa sehemu ya muonekano mpya wa soka la Tanzania.

KMC kwa sasa ndio wakombozi wa wilaya iliyokuwa inaonekana ni dhaifu katika soka jijini Dar es Salaam. Kinondoni wamekuwa na wakati mgumu kuwa na kikosi bora kinachowawakilisha katika ligi kuu au ligi nyingine kubwa.

Wakati fulani Villa waliwahi kujaribu, lakini mwendo wao ukawa wa kusuasua hadi wakaanguka kabisa. Safari hii, KMC ambayo inamilikiwa na Manispaaa ya Kinondoni imeonekana kwenda tofauti na kubadilisha mambo.

Safari hii wako Kagame Cup, wamewasili jijini Kigali wakiwa na kocha wao Mganda, Jackson Mayanja ambaye atachangia kuleta mabadiliko kama atapewa muda, ninaamini.

Walivyotua Kigali wanaonekana wana mpangilio mzuri kama timu na inawezekana wamejiandaa vema. Bado wanaweza wasifanye vizuri lakini hawatatoka kapa na watakuwa wametengeneza hamu nyingine ya kushiriki.

Hii maana yake ni kwamba watakaporejea Tanzania watacheza kwa nguvu na ushindani ili kuipata nafasi ya kwenda Kagame safari ijayo bila ya kuwa kwa msaada.

Pamoja na hivyo, kushiriki kwao Kagame kutawasaidia katika majukumu yao ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hiki wanachokijenga KMC, kitasaidia kukua kwao na kukua kwa Ligi ya Tanzania, maana yake kuna kitu kitaongezeka.

Kama utapata timu nyingine tano zenye mfumo kama wa Azam FC ambayo tumeona imekuwa na mchango mkubwa na baadaye kama KMC ambayo tunaiona inaamka vizuri, basi soka letu lina nafasi ya kubadilika kiasi kikubwa.


Ili maendeleo yapatikane, tusiwe na macho mawili tu. Yaani kuangalia Simba na Yanga pekee. Sisemi tuziue, badala yake tuzisaidie kuwa kubwa zaidi lakini tuwe na wakubwa wengine ambao tukiwajumlisha kwa kuwa na timu zaidi ya nane au tisa katika ligi, maana yake ushindani utaongezeka, viwango vitapanda na tutazalisha wachezaji bora watakaosambaa nchi mbalimbali duniani na mwisho kuwa na timu bora ya taifa.
SOMA NA HII  MBELGIJI WA YANGA AWASHANGAA WACHEZAJI WAKE KUPOTEZA MBELE YA KMC