Home Uncategorized EXCLUSIVE PART ONE: AMUNIKE ALIVYOVURUMISHA MATUSI KWA YONDANI, YEYE AMWAGA CHOZI

EXCLUSIVE PART ONE: AMUNIKE ALIVYOVURUMISHA MATUSI KWA YONDANI, YEYE AMWAGA CHOZI

Na Saleh Ally, Cairo
UKITAKA kumuuliza kila mmoja kuhusiana na mengi yaliyokuwa yanajitokeza ndani ya kikosi cha timu ya soka ya taifa maarufu kama Taifa Stars wakati ikishiriki michuano ya Afcon, utapata asilimia angalau 15 tu ya majibu sahihi.


Kawaida Watanzania tumefundishwa kuficha mambo na kuyazungumza taratibu kama sehemu ya kiburudisho na wakati mwingine huenda jambo fulani kama litawekwa wazi. Basi kuna nafasi ya kukomboa mengi ambayo yalikuwa tatizo.


Kikosi cha Taifa Stars kimecheza mechi tatu za makundi na kupoteza zote. Mechi ya kwanza ilikuwa ni 2-0 dhidi ya Senegal, mechi ya pili ambayo Stars ilionekana ina nafasi ya kufanya vizuri ikapoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Kenya.


Mwisho ilikuwa dhidi ya Algeria wakachapwa mabao 3-0. Kwa mara ya kwanza, wachezaji wa Stars, wengi wao wakaacha kuogopa na kucheza angalau mpira uliokuwa unaeleweka. Lakini makosa mfululizo mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Taifa Stars ikaruhusu mabao matatu ndani ya dakika 15.

Mechi dhidi ya Kenya, ndilo imewauma sana wengi ambao walipenda Tanzania ishinde. Inawauma kwa kuwa waliona timu ilistahili kushinda.


Kweli ilistahili kushinda na ilicheza soka linaloeleweka hadi kutangulia kufunga mabao mawili, Kenya wakisawazisha. Ndani ya mechi hiyohiyo, Tanzania ikaboronga tena na Kenya walipotanguliwa, ikawa safari imeisha.


Haya mengi ni yale yaliyokuwa yakishuhudiwa tokea nje ya kikosi. Likiwemo lile la taarifa la wachezaji kutaka kugoma wakidai dola 300 (Sh 687,233 )kwa siku. Lakini wachezaji wenyewe na baadhi ya viongozi walisema jambo hilo halikuwepo hata kidogo.

Pamoja na taarifa hizo za viongozi na baadhi ya wachezaji kulikataa, uchunguzi wangu ukabaini lilikuwepo na baadaye nitakuelezea namna ilivyokuwa, lilipoanzia na kwa nini lilitokea.

Wengi tulikubali kwamba wachezaji wetu bado wana viwango vya chini kupambana na wenzetu wanaotokea katika ligi mbalimbali kubwa. Lakini kama kungekuwa na muunganiko sahihi bila ya matatizo niliyoyagundua, huenda mambo yangeenda vizuri sana na hata kama ushindi mmoja au sare ingeweza kupatikana.


Kocha Emmanuel Amunike kwa muonekano ni mtu anayetia huruma sana. Kuna kila sababu ya kumheshimu kwa kuwa anaingia katika historia ya Tanzania kushiriki Afcon kwa mara ya pili ikiwa ni baada ya miaja 39, lakini uhalisia amekuwa tatizo kubwa na amechangia kwa kiasi kikubwa Stars kushindwa kufanya vema.

Niliamua kufanya uchunguzi ili nipate uhakika wa mengi ambayo nimeona yamekuwa athari na kama yatabaki siri, basi hakutakuwa na faida katika Afcon nyingine tukifanikiwa kwenda.

Uchunguzi nilioufanya kwa kina kupitia watu zaidi ya 12 wakiwemo walio ndani ya Stars, TFF lakini hata wale ambao waliishi na timu jijini Cairo. 

Kinachoshangaza ni kila kitu kutaka kufanywa siri kwa kuwa tu kuna hofu ya siasa ambayo imeingia ndani ya kikosi cha Stars kwa hiyo kila ambalo TFF wanaona wanaweza kusema kwa ajili ya kurekebisha, wanaona kama siasa zitaingia na kuleta mfarakano.


Kuna wanasiasa walianza kulumbana sababu ya timu hiyo ambayo wengi wao hawakuwa na msaada wowote. Lakini baadaye wengine wakaomba wapewe posho, waliponyimwa wakaishambulia timu. Hili nalo ni siri na hakuna anayejaribu kulisema kwa hofu ya kushikiliwa, kufikishwa mahakamani au kulalamikiwa mitandaoni.


Uchunguzi wangu umepita kwenye yote haya lakini leo ninaanza na Kocha Amunike ambaye kwa kiasi kikubwa naona ndiye alikuwa adui mkubwa wa Taifa Stars nikitoa asilimia 30 huenda hakuwa akijua kama anakosea na ninaweka asilimia 70, alikuwa anajua analolifanya.


Wakati wa mapumziko kwenye mechi ya Kenya, Amunike aliingia vyumbani, wengi wakitarajia kwa kuwa Taifa Stars ilikuwa inaongoza, angetoa maelekezo mazuri kuhusiana na kikosi nini cha kufanya kwenda kuongeza mabao na ikiwezekana kuwazuia kabisa Wakenya.


Muda wote wa mapumziko katika vyumba vya Taifa Stars kwenye Uwanja wa 30 June ulitumika kwa malumbano ya kupita kiasi. 

Kelele za wachezaji wakionyesha kukasirishwa na kile alichokisema kocha baada ya kumtukana beki Kelvin Yondani.


Moja ya tusi alilolitoa Amunike kwa Yondani ni kumuambia anacheza kama mwanamke. Kitu kilichowashangaza wengi kwa kuwa waliamini Yondani alipambana sana siku hiyo.


Kitendo hicho cha Amunike kutoa matusi na kebehi kwa wachezaji wake, tena beki aliyekuwa akionekana kuwa tatizo kwa washambuliaji wa Kenya, kiliwashitua wachezaji wengine wakataka kujaribu kuhoji, Amunike akawa mkali sana huku akisema maneno makali.


Kutokana na hali hiyo, Yondani akaanza kububujikwa machozi ikionekana dalili zote kwamba angeshindwa hata kucheza kipindi cha pili.


Baadhi ya wachezaji walianza kumbembeleza Yondani aliyekuwa amejiinamia kwa takribani dakika moja na nusu akilia kimyakimya huku akifuta machozi.

Nahodha Mbwana Samatta akaamua kuchukua jukumu hilo kama nahodha kwa kuzungumza tofauti na namna alivyokuwa amezungumza Amunike.

ENDELEA KUSOMA KESHO JUMAMOSI katika blogu hii ya SALEHJEMBE. USIKOSE.

MECHI ZA TAIFA STARS AFCON:
Vs Senegal 2-0
Vs Kenya 3-2

Vs Algeria 3-0
SOMA NA HII  HUYU HAPA MRITHI WA MIKOBA YA EYMAEL YANGA