Home Uncategorized SIRI NZITO KUTOKA ZESCO UNITED ZAWEKWA HADHARANI, NI FAIDA KWA YANGA

SIRI NZITO KUTOKA ZESCO UNITED ZAWEKWA HADHARANI, NI FAIDA KWA YANGA


Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila amewaambia mashabiki wa kikosi hicho wasiwe na presha watakapokutana na Zesco United kutokana na kumfahamu vizuri kocha wao, George Lwandamina ambaye amewahi kufanya naye kazi.

Mwandila ameweka wazi kuwa atatumia vitu anavyovijua kumpa bosi wake wa sasa, Mwinyi Zahera ikiwa ni sehemu ya kuwatoa wapinzani wao.

Yanga imepangwa kucheza na Zesco United ambayo kwa sasa inafundishwa na Lwandamina katika mchezo wa Hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao umepangwa kupigwa kati ya Septemba 13-15, mwaka huu.

Mwandila kwa nyakati tofauti amefanya kazi na Lwandamina, kwanza wakiwa Zesco United kisha baadaye Yanga ambapo walitwaa ubingwa wa mwisho wa klabu hiyo misimu mitatu nyuma.

Mwandila amesema kuwa kwake hana hofu ya kukutana na bosi wake huyo wa zamani kwenye mechi hiyo ambapo kwake atakuwa na kibarua cha kupambana naye kwa ajili ya kuifanikisha timu yake inapata ushindi na kusonga mbele.

“Ndiyo nimefanya kazi na Lwandamina na ninamjua vizuri kuwa mtu wa namna gani lakini kwa safari hii mimi nipo huku na yeye yupo huko. Kitu ambacho nitakifanya ni kuhakikisha timu yetu inasonga mbele kwa kufanya vizuri.

“Nitatumia kila ambalo ninalijua kuhusu mifumo na mbinu zake kwa ajili ya faida ya timu yetu, japo najua haitakuwa rahisi kwa sababu ya kutokuwa pamoja kwa miaka kadhaa lakini naamini kabisa vile ambavyo ninavijua bado anavitumia na hivyo vyote tutakaa na benchi letu la ufundi kwa ajili ya kuvijadili,” alisema Mwandila.

SOMA NA HII  MRITHI WA MIKOBA YA KATWILA ATOA LA MOYONI