Home Uncategorized MBELGIJI AGEUKA MBOGO, AWAPIGA STOP WACHEZAJI YANGA

MBELGIJI AGEUKA MBOGO, AWAPIGA STOP WACHEZAJI YANGA


KOCHA Mkuu mpya wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael, amewaambia wachezaji wake kuwa ni bora mpira upotee miguuni mwao lakini siyo kubutua mipira.

Mbelgiji huyo alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache kabla ya mchezo wa Ligi Kuu Bara na Singida United uliopigwa juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Liti zamani Namfua mkoani Singida ambao ulimalizika kwa Yanga kushinda mabao 3-1.

Kocha huyo tangu amepewa kibarua cha kukinoa kikosi hicho, ameonekana kuibadili timu hiyo kutokana na aina ya soka ambalo wanalicheza la pasi nyingi fupifupi wakati wakiwa na mpira wakishambulia goli la wapinzani wao. 

Yanga ikiwa inanolewa na Mholanzi Hans van Der Pluijm msimu wa 2014/15 na 2015/16, ilikuwa ikicheza soka la kuvutia huku wakipiga pasi nyingi fupifupi.

Kutokana na aina hiyo ya pasi nyingi, ukatungwa mtindo wa uchezaji wa Kampa Kampa Tena kutokana na soka hilo lililokuwa likipigwa,huku muasisi ni Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.

Soka hilo la pasi fupi lilitawaliwa na viungo wengi na kipindi hicho waliokuwepo ni Haruna Niyonzima, Deus Kaseke kipindi hicho anatoka Mbeya City kujiunga na Yanga, pamoja na Kamusoko mwenyewe ambaye hivi sasa yupo Zesco United ya Zambia.

Katika msimu huu, viungo waliopo ni Niyonzima, Kaseke, Pay Tshishimbi, Issa Mohamed ‘Banka’ na Bernard Morrison ambaye kwa muda mfupi amewateka mashabiki wa timu hiyo kutokana na uwezo mkubwa alionesha dhidi ya Singida, P pia upigaji wa pasi, kona na krosi safi.

Kabla ya Luc kutua kujiunga na Yanga, kocha msaidizi Charles Mkwasa aliyekuwa anakaimu nafasi ya Mkongomani Mwinyi Zahera ndiye aliyeanza kwa kuleta soka la pasi nyingi fupifupi wakiwa na mpira na hilo alilionyesha katika mchezo wa watani wa jadi, Simba baada ya vijana wake kucheza soka la kuvutia.

Ujio wa Luc, umeonekana kuendeleza aina hiyo ya soka katika michezo mitatu iliyopita ya ligi timu hiyo ilipocheza na Azam FC, Kagera Sugar na Singida United.

Kocha huyo katika mazoezi yake mara kadhaa ameonekana akiwataka wachezaji wake kupiga pasi fupifupi za haraka mara nne wakiwa ndani ya eneo lao la 18 kabla ya kutoka eneo hilo kwenda kushambulia goli la wapinzani wao.

Mbelgiji huyo mara baada ya mchezo wa Singida alisema: “Nimeanza kuona mabadiliko ya timu baada ya kuwaona wakifuata mfumo na aina yangu ya soka wanalotaka kucheza, kupiga pasi nyingi wakati tukiwa na mpira.

“Mara baada ya kuiona timu kule Zanzibar katika Kombe la Mapinduzi nilisema kuwa ninahitaji kuongeza kitu kidogo ambacho ndiyo hicho, nataka kuona timu ikicheza soka safi la pasi ambalo tayari baadhi ya wachezaji wameanza kuushika mfumo na aina ya soka ninalolitaka mimi.”
SOMA NA HII  YANGA YAZITAKA POINTI TATU ZA MWADUI FC