Home Uncategorized PACHA YA NCHIMBI NA MOLINGA ILIVYOIBUA MAKUBWA YANGA

PACHA YA NCHIMBI NA MOLINGA ILIVYOIBUA MAKUBWA YANGA


Mastraika wawili wa Yanga, David Molinga ‘Falcao’ na Ditrim Nchimbi pacha yao ni kama imeanza kukubali baada ya kila mmoja kumjua mwenzake wakiwa uwanjani, hapa wanakamilisha usemi wanaotumia Yanga kwa sasa “Wapeni Salaam”.

Hiyo imetokea ikiwa ni siku chache tangu Nchimbi amtengenezee Molinga bao moja kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar na baadaye na Ruvu Shooting michezo iliyopigwa jijini Dar es Salaam.

Hii ndiyo pacha ambayo inaonekana kuwa hatari zaidi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa na wanaonekana kuwa wanaweza kuipa timu hiyo ubingwa msimu huu.

Nchimbi ambaye alisajiliwa akitokea Polisi Tanzania, bado hajafunga bao lolote akiwa na timu hiyo, lakini uwezo wake wa kukaba, kukimbia na mpira unaonekana kuwa na faida kubwa sana kwa timu hiyo.

Uwezo wake umemsaidia Molinga kufunga mabao hayo na sasa ana mabao saba kwenye ligi hiyo akionekana kuwa anamsogelea kwa karibu zaidi kinara wa ufungaji kwa sasa kwenye ligi hiyo, Meddie Kagere wa Simba.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Luc Eymael, hivi sasa amembadilishia majukumu Nchimbi aliyekuwa akicheza namba 9 na kucheza namba 7 kama kiungo mshambuliaji.

Katika michezo ya hivi karibuni ya Ligi Kuu Bara, Nchimbi alikuwa akionekana na mpira pembeni mara nyingi anaangalia eneo la katikati ambalo anakuwa Molinga ambaye ni hodari wa kupiga mipira ya vichwa, pia akiwa na uwezo wa kufunga kwa miguu yote miwili.

Katika mchezo na Ruvu Shooting, Molinga kama angekuwa makini basi angefunga mabao zaidi ya moja kama angetumia vyema nafasi alizotengenezewa na Nchimbi ambaye alipiga krosi nyingi za kufunga lakini kutokana na umakini mdogo alizipoteza.

Kama Luc akiendelea kumtumia Nchimbi kucheza nafasi hiyo ya kiungo anayetokea pembeni, basi Molinga huenda akafi kisha idadi ya mabao 15 aliyoahidi aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo,  Mwinyi Zahera.

“Nchimbi ana kila sifa ya kucheza namba 7 kama kiungo mshambuliaji anayetokea pembeni ni kutokana na nguvu, kasi aliyokuwa nayo katika kulazimisha mabeki wa timu pinzani.

“Hivyo, Nchimbi ataendelea kucheza namba 7 na lengo ni kumtengenezea mabao Molinga anayetegemea krosi kutoka kwake,” alisema Luc.
SOMA NA HII  WACHEZAJI MSIBWETEKE, TIMU ZITUMIE MAPUMZIKO HAYA KUYAFANYIA KAZI MAKOSA