Home Uncategorized ANGALIA NAMNA SIMBA, YANGA WASIVYOJUA FAIDA YA WATU 60,000

ANGALIA NAMNA SIMBA, YANGA WASIVYOJUA FAIDA YA WATU 60,000




NA SALEH ALLY
KUNA kila sababu ya kusema kuwa hapa tulipofikia mechi hii ya Simba dhidi ya Yanga inapaswa kutumika kama jambo muhimu sana.


Hii inajulikana kama Dabi ya Kariakoo, mechi ambayo inawakutanisha Simba na Yanga wakiwa uwanjani kuchukuana lakini nje ndani ya nje ya uwanja kunakuwa na biashara kubwa kabisa.


Unaweza kuona watu 60,000 wanaokwenda Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushuhudia mchezo huo, kila mmoja akiwa na wazo moja tu la kuona timu ya yake inashinda.

Wakati wanamichezo hawa wapenda soka wanakwenda uwanjani wakitaka timu zao kushinda, biashara ya zaidi ya Sh milioni 500 hufanyika kwa siku moja tu kuwaruhusu watu hawa kupata huduma ya kuziona timu hizi maarufu zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Wanalipa viingilio ambavyo mgawanyo wake unatengeneza mapato kuanzia kwa Serikali ya Tanzania, klabu zenyewe, kampuni za ulinzi, wauza vinywaji, wafagiaji na kadhalika.


Unaona Uwanja wa Taifa unaingiza kitita cha fedha pale unapopata nafasi ya mechi hiyo kuchezwa kwenye uwanja huo. Serikali inapata pato lake kubwa kama kodi pia pale Yanga na Simba wanapokutana.


Kwa watu mbalimbali kupitia vikundi husika wanaingiza fedha zao kwa kiwango kikubwa kuliko wakati mwingine wowote, hata wale wanaouza jezi bila ya ruhusa nao huingiza fedha zao nyingi tu.


Kwa kifupi, riziki hutengenezwa kwa kiwango cha juu kabisa ukilinganishwa na wakati mwingine au kipindi wa mechi nyingine.


Ukiangalia kwa wengi mechi hii huwa tunaiangalia kwa jicho la kawaida, jicho la Simba dhidi ya Yanga nani atashinda na hatuitumii vizuri kwa maana ya sehemu kubwa au chanzo bora cha biashara.


Lazima Simba au Yanga wajipange, waangalie wanaweza kuingizaje fedha nyingi zaidi kupitia mechi hiyo kuliko kusubiri viingilio peke yake, jambo ambalo wamekuwa wakilifanya mara zote.


Waongeze mbinu nyingine, ikiwezekana klabu kufungua maduka madogo. Mfano Yanga inapokuwa mwenyeji basi kuwe na watu ambao wanauza bidhaa za klabu hiyo siku ya mechi hiyo kuanzia mapema kabisa.


Watu wanaouza wawe wanaingiza fedha zao na asilimia fulani inaingia katika klabu. Mara kadhaa nimebahatika kuwa katika viwanja kama Camp Nou, Old Trafford au Anfield, pale nje utakuta biashara hizi zinafanyika. Nililazimika kuuliza watu wanaouza jezi za klabu nje ya uwanja wakati klabu hizo zina madura makubwa katika viwanja hivyo, inakuwaje?


Nilifafanuliwa kuwa klabu inajua kwamba duka lake litaingiza fedha siku hiyo lakini inatanua biashara yake kwa kuwapa nafasi watu wengine wauze na wanagawana kwa asilimia.


Wanafanya hivyo kwa kuwa kwa wingi wa mashabiki siku hiyo si wote wanaweza kuingia dukani ukizingatia uwanja ni mkubwa na wengien wanaweza wasifike upande ambako duka lipo.


Hivyo wanaitumia fursa ya watu wengi kuwasogezea bidhaa na mwisho wale watu wanaouza wanapata na klabu inapata kwa wingi zaidi.


Jiulize klabu kama Manchester United au Barcelona inaona inaweza ikafanya hivyo, vipi Yanga au Simba zione zile fedha za viingilio pekee ndio zinatosha kwao, maana yake hakuna ubunifu wa kutosha wa vitengo vyao vya masoko na kama vipo, basi ni kama vipo tu.


Vitengo vya masoko vya klabu hizo, vinaweza kuwa vinafanya kazi ya ubunifu kuelekea katika mechi hiyo kwamba zinaweza kutengeneza fedha kwa njia zipi.


Kwa kusoma namna hali ilivyo, basi kama ni wataalamu wa masoko wanaweza kuamua kufanya jambo sahihi kwa kuhakikisha zinafaidika na umma unaokwenda uwanjani siku hiyo ya mechi.


Umma huo ni nadra kupatikana kwa wepesi, lazima kuwe na kitu haa kinachowalazimisha watu kufika eneo husika. Kuwashawishi kufika eneo husika si kazi ndogo, hivyo kuutumia ni jambo jema.


Klabu isiende uwanjani kufuata pointi tatu pekee, badala yake iandae pointi nyingine tatu nje ya uwanja ambazo zitaendelea kupunguza klabu hizi tajiri kwa rasilimali kuendelea kuwa tegemezi.


Simba na Yanga kwa sasa wala hazina sababu ya kuwategemea Mo Dewji au GSM katika kile kiwango cha kutaka kuwaangukia.


Badala yake wao ndio walipaswa kuwa wanaomba kuwa upande wa Yanga na Simba kutokana na namna klabu zilivyo na nafasi ya kuwatangaza na kuwatangazia biashara zao.


Bila shaka utakuwa umenielewa, ninamanisha hasa kwa kuwa nimekuwa nikikerwa na kuona kitu chenye nguvu kinawanyenyekea na kuwabembeleza kwa kuwa tu walio ndani yake hawana ubunifu.


Walio ndani ya klabu hizi wanaamini malumbano na sifa ndio mafanikio. Bado hawajaelewa, kukusanya watu 60,000 si jambo dogo, si jambo la kawaida na ukifanikiwa kufanya hivyo basi watumie watu hao waliokufuata au kuwafuata kujiinua zaidi kwa ajili ya biashara yako.
SOMA NA HII  TABU NYINGINE YAIANDAMA YANGA, MMOJA NJE KWA MUDA USIOJULIKANA