Home Uncategorized CORONA KWA KOCHA ARSENAL, BEKI JUVENTUS NI UJUMBE HADI LIGI KUU BARA

CORONA KWA KOCHA ARSENAL, BEKI JUVENTUS NI UJUMBE HADI LIGI KUU BARA





Na Saleh Ally
USIKU wa kuamkia jana imetangazwa kuwa beki wa klabu kigogo ya Italia, Juventus amebainika kuwa anaugua ugonjwa wa Covid-19 maarufu kama Corona.


Huyu ni Daniele Rugani ambaye ana umri wa miaka 25. Bado hakujawa na kila kitu hadharani lakini klabu hiyo kongwe, imethibitisha.

Wakati Rugani akikutana na msala huo, tayari Seria A imesimamishwa kwa muda ili kupisha janga hili kubwa kwa kuwa Italia ndio nchi iliyoathirika zaidi na Corona baada ya China.

Baada ya Rugani kupata maambukizi ya Corona, inaonekana kuwashitua watu wengi sana. Huenda walikuwa wakiamini kama Watanzania wengi kwamba watu fulani hivi hawawezi kuambukizwa Corona.

Wakati tukiamini huenda itaishia hapo, Corona imeonekana kuwa tishio baada ya Kocha Mikel Arteta wa Arsenal na badaye beki Callum Hudson-Odi naye kutangazwa kuwa wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo hatari wa Corona.


Inawezekana tuliamini Corona ni ya nchi fulani au eneo fulani na huku kwetu kuna ugumu, si sahihi. Dunia ipo matatani na vema kusaidia kulimaliza hili kwa mpangilio ulio sahihi tukishirikiana kwa ukaribu na wana michezo, ni sehemu muhimu.


Kwa Bara la Ulaya, Italia na hasa upande wa Kaskazini mwa nchi hiyo ndio kuna matatizo makubwa sana.

Kabla ya hapo, hatua kadhaa zilichukuliwa kuhakikisha baadhi ya michuano inasimamishwa na hii si soka tu hata tenisi, mbio za magari na michezo mingine imesimamishwa.


Hii maana yake ugonjwa huu si unapt mbinguni na Watanzania hatuwezi kukumbana nao. Jambo muhimu ni kujipanga na kujiandaa kwa tahadhari ambayo inajulikana, tahadhari ni sehemu ya kinga na unajua kinga ni bora kuliko tiba.


Tumeona China walivyopambana na virusi hivyo vya Corona, ni wazi kuwa ni vikali, visumbufu na tatizo kubwa, hivyo ni lazima kuwa makini kabla havijaingia.


Wanamichezo wanaweza kuwa imara zaidi kwa kuendelea kusisitiza watu kuwa makini kwa kuwa kama walianza wananchi wa kawaida, wakafuatia hadi viongozi kama mawaziri tumeona Uingereza, Iran na kwingineko, vipi ishindikane hapa kwetu Tanzania?

Ninaamini sote tunaomba isije ikawa hapa kwetu lakini tunajua kwamba kuomba pekee hakutoshi ni lazima kuwe na mpango mkakati na vyama vya michezo na hasa kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linapaswa kuwa mshauri na mtekelezaji namba moja na tahadhari iwe kubwa.


Nimeona zile juhudi za kuzuia kupeana mikono, si vibaya ingawa kimtazamo nashindwa kuelewa vizuri kwa kuwa wachezaji wamekuwa wakivutana, kukumbatiana na hata kuangukiana, vipi hapo?


Hivyo ni vizuri kama itawezekana, vyama vya michezo pia mashirikisho vikakutana chini ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa pamoja na kulijadili suala la Corona kama sehemu ya tahadhari.

Katika nchi yetu na nchi nyingi sana, mikusanyiko mikubwa zaidi ni ya kimichezo. Angalia Jumapili iliyopita, Yanga na Simba zilikutana na kukutanisha zaidi ya watu 60,000 ambao kuwapata kwa ajili ya siasa si jambo dogo, inatokea aghalabu katika uchaguzi mkuu ambao unahusisha na upigaji kura zikiwemo za rais.

Tanzania si kisiwa, kujiandaa si kutisha na tuachane na kuamini tukizungumzia tutakuwa tunawatisha watu, badala yake tuwe huru na wazi lakini si tuyakuze.

Wanamichezo wana nafasi kubwa ya kufikisha ujumbe katika jamii. Kwa mnaokumbuka wakati fulani wanamichezo tulitumika kuzungumzia kuhusiana na tatizo la Ukimwi na ilikuwa kuna wepesi kufikisha ujumbe.


Katika Corona pia inawezekana kwa kuwa Tanzania si kisiwa na kama wenzetu wako hatarini na kwa kuwa tunaishi nao, nasi tuko hatarini pia, ndio maana nasisitiza, suala la tahadhari halina mjadala.

Wanamichezo waendelee kutengeneza ujumbe wa tahadhali si kwa kutisha, si kwa kukuza, badala yake kukumbusha na kutahadhalisha kuhusiana na ugonjwa huu.


Mambo ya msingi kuwaambia watu kwa kuwapa ujumbe wa kuwa makini, ujumbe kuwa ugonjwa huu hauchagui mtu na kadhalika lakini kuhakikisha jamii inakuwa makini bila ya kulikuza hili.

Pia kuwasisitiza watu kuwa suala la taarifa Corona ipo au haipo si la kwao, waziachie mamlaka husika ndio zenye maelezo sahihi na si kila mmoja ageuke mtoa taarifa, jambo ambalo si sahihi hata kidogo.



SOMA NA HII  KUHUSU DABI YA KARIAKOO HAWA SASA NDIO WAKONGWE WENYEWE