Home Uncategorized MCHEZO MZIMA WA YANGA KUMALIZANA NA MBAO FC JANA TAIFA UPO HIVI

MCHEZO MZIMA WA YANGA KUMALIZANA NA MBAO FC JANA TAIFA UPO HIVI


YANGA jana ilimalizana na Mbao mapema kabisa Uwanja wa Taifa kwa ushindi wa mabao 2-0 yaliyowapa pointi tatu muhimu.
David Molinga mshambuliaji wa Yanga alianza kuwanyanyua mashabiki  dakika ya 26 kwa mkwaju wa penalti baada ya Fei Toto kuchezewa rafu ndani ya 18, guu lake la kulia lilimshinda  mlinda mlango wa Mbao FC Rahim Abdalah aliyeishia kuokota mpira nyavuni.
Kipindi cha pili Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi ambapo ilibidi isubiri mpaka dakika ya 81 kufunga bao la pili kupitia kwa Patrick Sibomana aliyefunga bao hilo kwa pasi ya Tariq Seif iliyomchanganya mlinda mlango wa Mbao.
Mbao pia ilifanya mashambulizi kupitia kwa Wazir Junior ambaye alikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Yanga waliokuwa wakiongozwa na Kelvin Yondan.
Yanga ilifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake jana ambapo sura mpya ziliibukia Taifa kwenye mchezo huo ambao ni pamoja Patrick Sibomana, Mrisho Ngasa,Farouk Shikalo na Papy Tshishimbi ambao wote waliukosa mchezo uliopita dhidi ya Alliance FC .
Majembe ya kazi kama Metacha Mnata, Erick Kambamba, Bernard Morrison yalianzia benchi kuusoma mchezo huo wakiivutia kasi mechi yao ya Machi 8.
Huu unakuwa ni ushindi wa pili mfululizo Yanga wanaupata walianza mbele ya Alliance FC kwa kuitungua mabao 2-0 Uwanja wa Taifa na jana ilikuwa zamu ya Mbao FC zote kutoka kanda ya ziwa.
Molinga alionekana mwenye furaha baada ya kufunga bao lake la 8 ndani ya ligi huku akiwaambia mashabiki kwa ishara kwamba watulie kuna jambo kubwa litafanyika kwenye uwanja huo.
Machi 8, Yanga itawakaribisha Simba Uwanja wa Taifa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao utakuwa ni mzunguko wa pili  na inaonekana kwamba kwa ushindi walioupata jana itaongeza morali na nguvu kwa wachezaji wao. 
SOMA NA HII  KILICHOWAFANYA YANGA WAKAMPA DILI MSERBIA HIKI HAPA