Home Uncategorized VIWANJA HIVI NI ADUI MKUBWA WA MAENDELEI YA SOKA TANZANIA

VIWANJA HIVI NI ADUI MKUBWA WA MAENDELEI YA SOKA TANZANIA




NA LUC EYMAEL
NINA uzoefu mkubwa na soka la Afrika kwa kuwa nimefundisha zaidi ya nchi tano na nimekuwa nikijifunza mambo mengi sana.


Ukisikia Kocha Eymael, kwangu Afrika ndio nyumbani namba mbili baada ya Ubelgiji na nimepata nafasi nyingi za kuzungumza au kuchambua mambo kadhaa katika vyombo mbalimbali vya habari, kwa Tanzania hii ni mara ya kwanza.


Tanzania ni nchi ambayo naendelea kujifunza mambo mengi sana na ninaona, naweza kusema ni mambo magumu ninayokutana nayo lakini yale yanayoniimarisha kujua ninafanya jambo gani.


Nilitaka kuja Yanga takribani miaka minne au mitano iliyopita lakini haikutokea, baada ya hapo nikaendelea na maisha mengine nikifanya kazi katika nchi nyingine za Afrika.


Kwangu, Afrika Mashariki tayari nimefanya kazi katika nchi nne kwa maana ya DR Congo, Rwanda, Kenya na sasa Tanzania. Kabla nilikuwa Gabon na Afrika Kusini ambako naweza kusema nimeona kuna tofauti kidogo.


Tokea nimekuja Tanzania, kuna mambo kadhaa ambayo naona hayana tofauti na nchi za Afrika nilizopita lakini yapo yale ambayo ninaona yana tofauti na ingependeza kuona yanafanyiwa mabadiliko makubwa ili kuleta mabadiliko kwa kuwa katika mpira na hasa viwanja.


Kilio changu ni viwanja kwa kuwa umenipa wakati mgumu sana kwa sababu kama ukicheza katika uwanja mzuri basi itakuwa ni Dar es Salaam, jambo ambalo si sahihi hata kidogo.


Hii iliwahi kunikukuta wakati nikiwa DR Congo wakati naifundisha AS Vita, mtacheza mechi vizuri na kwa ushindani wa hali ya juu pale mnapokuwa mnacheza pale Kinshasa, baadaye utasafiri hadi Lubumbashi kwenda kuivaa TP Mazembe, napo mambo ni mazuri sana na unacheza vizuri katika kiwango bora na hata kwenye uwanja mzuri na vyumba vya kubadilishia nguo ni katika kiwango bora kabisa.


Ajabu ulikuwa ukienda katika baadhi ya miji unachanganyikiwa, hata sehemu ya kubadilishia nguo ni shida. Unaambiwa hapa ndio vyumba vya kubadilishia nguo, ukiangalia hauwezi ukaamini namna hali ilivyo. Wakati mwingine ni hema tu limewekwa, jambo ambalo si sahihi na Fifa haikubaliani na haya mambo.


Mwaka 2010 na 2011, nakumbuka ilikuwa Gabon, nako ilikuwa hivihivi, hakuna sehemu ya kubadilishia nguo wakati mwingine lakini sasa hii ni Tanzania na huu ni mwaka 2020 mambo hayapaswi kuwa vilevile, hili si jambo sahihi na lazima lifanyiwe kazi kama kweli tunataka maendeleo mpira.

Hivi juzi nilisafiri na timu kwenda kucheza mechi dhidi ya Namungo, hakika haikuwa  sahihi hata kidogo. Wakati mwingine unaweza kuwalaumu wachezaji lakini kuna mazingira unalazimika kuwaonea huruma. Kuna wakati tukiwa njiani unashangazwa kabisa na hali ilivyo, maana hauwezi ukatulia kwenye kiti angalau kwa dakika moja, mnarushwa vibaya sana.


Barabara mbovu sijawahi kuona, tulikuwa tukirushwa sana, na tulifika tukiwa tumechoka sana. Kwangu lilikuwa ni jambo jingine jipya la kujifunza lakini kwa maana ya wachezaji kucheza wakiwa na kiwango kizuri, unatarajia litatokea lakini haiwezi kuwa asilimia mia.


Ukiachana na uchovu wa barabarani, uwanja unaokwenda kucheza ukiwa kwa nje unaonekana ni mzuri lakini ingia ndani, mpira unadunda utafikiri unakaanga pop corn, vipi mnaweza kucheza katika kiwango kizuri.


Kiwango kizuri kinabaki jijini Dar es Salaam pekee baada ya hapo ni viwanja vichache sana, hili si jambo sahihi hata kidogo kwa kuwa mpira hauwezi kukua kwa kupitia Dar es Salaam pekee huku sehemu nyingine zote zikiwa na kiwango kibovu.


Kitu ambacho watu wanaweza kujifunza ni kwamba mimi kocha wa klabu ni sehemu ya maendeleo ya mpira wa Tanzania. Hili jambo lazima watu wote waelewe kwa kuwa ninawafundisha wachezaji wa Kitanzania na kama kocha nitataka kukuza kiwango chao.


Ninapokuza kiwango chao kikapanda, maana yake ninaisaidia Tanzania kuwa na wachezaji bora kabisa. Angalia nilipokuja, idadi ya wachezaji wa Yanga imeongezeka kwenda kwenye timu ya taifa.


Binafsi najivunia kwa kazi nzuri, kama kocha ukiwa na wachezaji wengi zaidi katika timu ya taifa wanakwenda kufika hadi saba, si jambo dogo maana yake kuna viwango vya wachezaji wako vimekua na wanapokwenda kwenye timu ya taifa wanapata molari zaidi ya kufanya vema.


Najua utakuwa na hamu ya kunisikia nikizungumza mengi kuhusiana na mpira wa Tanzania ambao naendelea kujifunza mengi.


Kesho Jumamosi nitazungumzia suala kuhusiana na namna ambavyo tumekuwa tukipambana, mambo yanavyokwenda, ninachotaka baadaye na pia kuhusiana na mechi yetu dhidi ya Simba ilivyokuwa.
SOMA NA HII  MATOKEO YA MECHI ZA LEO, VPL