Home Uncategorized MIRAJI ATHUMAN- NIMEREJEA UPYAAA

MIRAJI ATHUMAN- NIMEREJEA UPYAAA

MSHAMBULIAJI wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Miraji Athuman, amesema mazoezi ya wiki mbili yatamfanya arejee katika ubora wake ule ule ambao alikuwa nao kabla ya kupata majeraha.

Akizungumza na gazeti la NIPASHE  jijini Dar es Salaam jana, Miraji alisema anafanya mazoezi ya kunyonga baiskeli kwa ajili ya kujiweka sawa kabla ya kurudi rasmi uwanjani.

Miraji alisema mazoezi hayo ya wiki mbili yatamfanya arudi katika kiwango chake kilichozoeleka na lengo ni kuisaidia Simba kutimiza malengo.

“Nilipewa mazoezi ambayo naendelea kufanya ili kurejea kwenye ubora wangu, kwa muda wa wiki mbili nitakuwa ninaendesha kibaiskeli maalumu kwa ajili ya kujiweka sawa,” alisema Miraji.

Aliongeza mazoezi hayo yatamfanya awe kwenye nafasi na ubora wa juu kuliko hapo awali na baada ya kumaliza programu hiyo atasubiri maelekezo mengine kutoka kwa daktari wao.

“Ninamshukuru Mungu afya yangu imeimarika, nimefuata maelekezo yote niliyokuwa napewa na daktari wangu, ninajuwa mashabiki wangu wana kiu ya kuniona, nawaahidi nitarejea kwa kasi ile ile,” Miraji alisema.

Miraji alipata majeraha ya mfupa mdogo katika mguu wa kulia ambayo aliyapata akiwa na timu ya Taifa (Taifa Stars), na baadaye alijitonesha majeraha hayo alipokuwa na klabu yake kwenye mchezo wa fainali wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo Simba ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Simba ndio vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 71 baada ya kushuka dimbani mara 28 na inahitaji pointi 12 ili itetee taji ambalo inalishikilia.

SOMA NA HII  GSM WAZIDI KUSHUSHA NEEMA YANGA..WASAINI MKATABA MPYA UTAKAOWAPA YANGA MABILIONI