Home Uncategorized YANGA NA TSHISHIMBI..MAMBO NI BAMBAM..!!

YANGA NA TSHISHIMBI..MAMBO NI BAMBAM..!!

HATIMAYE uongozi wa Yanga umefanikiwa kukamilisha mchakato wa kumwongezea mkataba mpya kiungo wake wa kimataifa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Papy Tshishimbi, ambaye inadaiwa alikuwa anawindwa na watani zao, Simba, imefahamika.

Mbali na kukamilisha usajili huo, Yanga pia imemaliza tofauti iliyokuwapo na wadhamini wao, Kampuni ya GSM, baada ya kufikia muafaka katika kikao kilichofanyika juzi jijini Dar es Salaam.

Taarifa zilizopatikana jijini jana zinasema Tshishimbi amesaini mkataba mpya wa miaka miwili akiwa ni mmoja wa wachezaji waliopendekezwa kubakia na Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael.

Akizungumza na gazeti hili jana, Tshishimbi alisema amesaini mkataba wa kuendelea kuitumikia Yanga baada ya klabu hiyo kumpatia dau alilowatajia.

“Tayari tumeshamalizana, biashara imekwisha, Wanayanga bado tuko pamoja,” alisema kwa kifupi kiungo huyo Mkongomani.

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said, alisema tayari tofauti zilizokuwapo kati yao na Yanga zimemalizika na sasa hivi wanajipanga kuhakikisha klabu hiyo inaimarisha kwa kuanza na mchakato wa usajili.

Said alisema wameanza na Tshishimbi na wanaahidi kikosi cha timu hiyo itakuwa imara ili msimu ujao waweze kuchukua ubingwa wa Tanzania Bara na Afrika.

Aliongeza chini ya GSM, Yanga inajipanga kusajili kikosi kitakachokuwa na uwezo wa kupambana kuwania taji la Afrika kwa kuwapatia wachezaji mahitaji yote muhimu ili wafikie malengo yao.

“Hili suala la kukosa ubingwa mara tatu mfululizo linaumiza sana, hivyo tushirikiane kuhakikisha tunafanya usajili mzuri na huku tukipambana kubakiza wachezaji ambao wamemaliza mkataba na bado wanahitajika,” Said aliongeza.

Naye Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, amewataka wanachama wa klabu hiyo kujiandaa na mfumo mpya wa uwekezaji ambao utaibadilisha klabu hiyo.

Nugaz alisema Yanga itashirikiana na maofisa wa La Liga katika mchakato huo wa mabadiliko ambao utawaondoa kwenye mfumo tegemezi.

SOMA NA HII  YANGA KUISHUSHA SIMBA KILELENI