Home Uncategorized


Na Saleh Ally
TIMU pekee ilikuwa inaweza kuizuia Liverpool kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England ni mabingwa watetezi, Manchester City ambao wanazidiwa kwa pengo la pengo la pointi 25 katika msimamo.


Maana yake ingekuwa miujiza kuizuia Liverpool ambayo ilikuwa imebakiza mechi tisa mkononi kutangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu England baada ya zaidi ya miaka 20.


Hamu kubwa ya Liverpool ni hiyo, kombe hili limewaponyoka kwa zaidi ya miaka 20 hadi kufikia kuipa nafasi Manchester United kubeba ubingwa huo mara nyingi zaidi yao.


Wakati ndiyo ulikuwa umefika bahati mbaya kabisa kumeuibuka maambukizi ya Covid-19 na kusababisha hofu kubwa duniani kote ikiwemo England ndani ya Uingereza.


Hofu hiyo imesababisha kusimamishwa kwa michezo mbalimbali duniani kote zikiwemo ligi zote za soka hata zile maarufu ligi hiyo maarufu kwa jina la Premier League au EPL.


Juzi, Ufaransa maarufu kama Ligue 1 ilikuwa ligi kuu kubwa ya kwanza ya soka kati ya zile tano za Ulaya kutangaza kumaliza msimu na kuwapa kombe waliokuwa vinara yaani PSG. Tayari mjadala umezuka kama kweli ligi nyingine nne zilizobaki zitaweza kurejea.


Ligi hizo ni Bundesliga, Serie A, La Liga na EPL yenyewe. Tayari Bundesliga wametangaza kurejea uwanjani Mei 9, zoezi ambalo linaonekana litakuwa katika usimamizi wa karibu kabisa na wataalamu wa afya kwa kuwa tayari wameanza na timu ziliporejea mazoezini.


EPL nao wameona inawezekana na wameruhusu timu kurejea mazoezini wakiwa na matumaini ya kumalizia mechi zilizobaki kwa kuwa ni 10 kwa Manchester City pekee na zilizobaki ni mechi tisa tu.


Kama zitachezwa mbili kwa kila wiki, ndani ya mwezi mmoja na nusu huenda kila kitu kikawa tayari lakini itawezekana baadhi ya wiki zikachezwa tatu ikiwa ni sehemu ya kuongeza kasi ya kumaliza.


Vyovyote vile kama ligi inarejea au la, Liverpool walikuwa na asilimia 90 ya kuwa mabingwa wa England kwa sababu za msingi na hata ikitokea ligi hii haitaendelea, kuwanyima ubingwa itakuwa ni muujiza wa kushangaza.


Pengo la pointi 25, maana yake ni hivi; kama Manchester City wangeshinda mechi zao 10 zilizobaki wangekuwa na pointi 87. Tayari Liverpool walikuwa kileleni wakiwa na pointi 82, maana yake tofauti ni pointi tano tu ambazo walikuwa na uwezo wa kuzipata katika mechi mbili dhidi ya Everton wakiwa ugenini na Crystal Palace wakiwa nyumbani.


Mechi mbili zilizokuwa zinafuata baada ya hapo ilikuwa dhidi ya Manchester City ambayo ilipangwa kuchezwa Aprili 5, Liverpool wakiwa ugenini Etihad na ile ya Brighton nyumbani Afield.

Leo Mei 2, Liverpool walikuwa na mechi jijini London dhidi ya Arsenal. Ninaamini ingekuwa ni mechi ya kujifurahisha kwa kuwa lazima wangeishakuwa mabingwa kutokana na kasi walikuwa wanakwenda nayo.


Hadi ligi inasimamishwa, mechi zao nane zilizopita walikuwa wameshinda saba na kupoteza moja, wakizichapa Man United (2-0), Wolves (2-1), West Ham (2-0), Southampton (4-0),  Norwich City (1-0), West Ham (3-2) na Bournemouth (2-1) huku wakiwa wamepoteza mechi moja kwa kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya Watford.

Kwa mwendo huu, ndani ya mechi 9 hauwezi kusema wangeshindwa kupata pointi sita pekee ili kuwa mabingwa na huenda walikuwa karibu kupita kiasi, jambo ambalo linawachanganya zaidi wanapoona ligi hiyo inashindikana kurejea.


Inawezekana ukawa shabiki wa timu nyingine ya England na usingependa kuona Liverpool wakipewa ubingwa na ungependa kuona ligi inarejea. Kwa kuwa ni burudani ni jambo zuri ili angalau kuonyesha maisha ya kawaida yanaendelea.


Kama itashindikana, ligi ikaishia hapo, msimamo unatusuta sote kusema Liverpool haistahili kupewa ubingwa kwa kuwa pengo lao la “Social Distancing” ya ukweli, linaonyesha watastahili na kupewa ubingwa ni haki yao.
SOMA NA HII  NYOTA HUYU ALIYEKIPIGA ULAYA YUPO MBIONI KUTANGAZWA YANGA