FRANCIS Kahata ndiyo jembe la kazi la Simba ambalo inaelezwa kuwa linatua leo kuungana na mabingwa hao watetezi kuendelea mbio za kuufukuza ubingwa zinazotarajiwa kurejea Juni Mosi.
Wakati Ligi Kuu Bara ikisimamishwa Machi 17 kutokana na janga la Virusi vya Corona, Kahata raia wa Kenya alisepa Bongo na kuibukia nchini kwao kuchukua mapumziko pamoja na nyota wengine ambao ni Clatous Chama (Zambia), Sharaf Shiboub (Sudan), Meddie Kagere (Rwanda) ambao wanatarajiwa kurejea ndani ya wiki hii huku leo habari zikieleza kuwa Kahata anatua.
Rekodi za Kahata ndani ya Simba iliyofunga jumla ya mabao 63 ni matata kwani amehusika kwenye jumla ya mabao 10 akitoa jumla ya pasi sita na kufunga jumla ya mabao manne ana uwezo wa kutumia miguu yote miwili pamoja na vichwa.
Hawa hapa walikutana na pasi zake:-Meddie Kagere mbele ya Azam FC alipewa pasi wakati Simba ilishinda bao 1-0, Miraj Athuman na Tairone Santos walimaliza pasi za Kahata wakati wakiichinja mabao 3-0 Ruvu Shooting ,John Bocco aliimaliza Lipuli kwa bao 1-0 akipokea pasi yake ya guu la kushoto.
Gerson Fraga aliwaangamiza KMC kwa mabao 2-0 akitumia pasi moja ya Kahata na Ibrahim Ajibu bao lake alilowafunga Polisi Tanzania alimalizia pasi ya Kahata wakati Simba ikishinda mabao 2-0.
Aliwatungua Lipuli kwa guu la kulia wakati Simba ikishinda mabao 4-0, Ndanda FC kwa free kick kwa guu la kushoto wakati Simba ikishinda mabao 2-0, aliwatungua Namungo wakati Simba ikishinda mabao 3-2 kwa kichwa, Biashara United wakati Simba ikishinda mabao 3-1 kwa guu la kulia.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema kuwa jitihada zinaendelea kuwarudisha nyota wao huku leo akitarajiwa kutua mmoja.