Home Uncategorized HAWA HAPA MBEYA CITY, ANGUKO LAO NA MAFANIKIO YAO YAMEJIFICHA HAPA

HAWA HAPA MBEYA CITY, ANGUKO LAO NA MAFANIKIO YAO YAMEJIFICHA HAPA


UKIZUNGUMZIA timu ambazo ndani ya Ligi Kuu Bara zilipanda kwa mbwembwe kibao na wengi kuzitabiria makubwa hapo baadaye jina la Mbeya City huwezi kuliweka kando.
Klabu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Mji ya Wilaya ya Mbeya ilianzishwa mwaka 2011 ipo Nyanda za Juu Kusini.
Ilikuwa na mwanzo mzuri na iliweza kujikusanyia mashabiki wa kutosha ambapo ilikuwa ni fahari kwa wana nyanda za juu kusini kuvaa jezi ya Mbeya City na kupita mtaani wakitamba.
Kushiriki Ligi Kuu Bara
Kwa mara ya kwanza ilianza kushiriki ligi msimu wa 2013/14 ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu kibindoni na pointi zake 49.
Ilishinda mechi 13 sare mechi 10 na ilipoteza mechi tatu, iliwapoteza kwenye ramani Simba ambapo ilimaliza msimu ikiwa nafasi ya nne kibindoni na pointi zake 38.
Mbeya City ilitumia dakika 2,340 msimu wake wa kwanza uwanjani ambapo ilifunga jumla ya mabao 33 na kufungwa  20.
Ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Juma Mwambusi ilikuwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 70 na kuruhusu ngome yao kupenywa kila baada ya dakika 117.
Itakumbukwa kuwa Mbeya City ile ilikuwa inakuja na mashabiki wa kutosha kwenye magari kutoka Mbeya mpaka pale Taifa kuipa sapoti, ilikuwa ni mwana ukome.
Uwanja wao
Mbeya City wanatumia Uwanja wa Sokoine. Una uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000.
Hiki hapa kilijificha nyuma ya mafanikio
Mwambusi ambaye alikuwa Kocha Mkuu wakati ule wa Mbeya City iliyokuwa inatesa kila kona ya Bongo anaweka wazi kuwa wakati huo alikuwa anaiona Mbeya City ya kawaida kwani haikuwa kwenye ubora wake.
“Nilikuwa nimetoka kuinoa Tanzania Prisons wakati huo nikakabidhiwa timu ya Mbeya City, imani yangu ni kwamba Tanzania Prisons ilikuwa ya moto kuliko Mbeya City iliyomaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu.
“Mambo makubwa matatu yaliibeba, nadhani wengi bado walikuwa shule na wengine kwa sasa wanasikia habari za ile Mbeya City. Jambo la kwanza ilikuwa maandalizi makini kwa wachezaji, pili uongozi bora na tatu kufanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa.
Paul Nonga ambaye kwa sasa anakipiga Lipuli alikuwa mmoja wa wachezaji msimu wa kwanza amesema kuwa wachezaji walikuwa na nidhamu nje na ndani ya uwanja.
Usafiri wao balaa
Miongoni mwa timu ambazo zina usafiri binafsi ni pamoja na Mbeya City.
Basi hilo walikabidhiwa Desemba 2, 2015 na mdhamini wao wa wakati ule Binslum lenye thamani ya zaidi ya shilingi za kibongo milioni 180  ambalo lina sehemu ya kukaa kwa baadhi ya viongozi na wachezaji kufanya kikao cha ndani.
Hawa hapa wamepeta
Juma Kaseja kwa sasa anakipiga KMC, Mrisho Ngassa yupo zake Yanga, Juma Nyosso anakipiga Kagera Sugar, Eliud Ambokile ambaye mpaka anasepa Mbeya City msimu wa 2018/19 alitupia mabao 10 na kwa sasa anakipiga ndani ya TP Mazembe ya Congo.
Anguko lake
Msimu huu wa 2019/20 ilianza kwa kusuasua na ilisababisha kocha Mwambusi kubwaga manyanga. Sare ya bila kufungana na Alliance, Uwanja wa Nyamagana ilimuumiza kwani walikuwa wapinzani wapo tisa uwanjani baada ya kipa wa Alliance kulimwa kadi nyekundu pamoja na mchezaji mmoja ila ngoma ilikamilika kwa sare tasa.
Mwambusi amefunguka na kuweka wazi kuwa ilikuwa ni kinyume cha yale mambo matatu yaliyompa mafanikio.
“Nilirejea Mbeya City msimu huu timu ikiwa haina muda mrefu wa maandalizi na pia kulikuwa na tatizo la pesa. Kutoelewana na baadhi ya viongozi pamoja na wachezaji kushindwa kumalizia nafasi za wazi.
“Wakati napewa timu niliwaambia tunatakiwa tuwe na subira, matokeo ya mwanzo hayatakuwa mazuri kwani mimi nafundisha kwa utaratibu na mpira una hatua zake. Mwisho wa siku nikaona hawataweza kuwa wavumilivu na matokeo ambayo tunayapata nikaamua kujiweka kando.
Ilipo sasa
Kwa sasa Mbeya City ipo chini ya Kocha Mkuu, Amri Said ikiwa nafasi ya 17 kibindoni ina pointi 30 baada ya kucheza mechi 29. Imeshinda mechi saba sare 10 kichapo mechi 13 na imebebeshwa furushi la mabao 35 huku wao wakifunga mabao 22 na mtupiaji wao namba moja ni Peter Mapunda mwenye mabao tisa.
SOMA NA HII  KESHO NDANI YA CHAMPIONI IJUMAA USIPANGE KUKOSA NAKALA YAKO