Home Uncategorized TAYARI TALIB HILAL AMEFUNGUA NJIA, WANAMICHEZO RUDISHENI NYUMBANI VITA DHIDI YA CORONA

TAYARI TALIB HILAL AMEFUNGUA NJIA, WANAMICHEZO RUDISHENI NYUMBANI VITA DHIDI YA CORONA



NA SALEH ALLY
NILIKUWA naangalia kiungo kinda wa FC Barcelona, Moussa Wague alivyoamua kutoa misaada ya chakula na mafuta tani 12 katika eneo alilozaliwa la Bignona nchini Senegal.


Amesema misaada hiyo ni kujiandaa na vita dhidi ya Covid 19 ingawa hadi sasa hakuna kesi hata moja katika eneo la Bignona. Wague ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo katika klabu ya Nice ya Ufaransa amesema ni vizuri kuanza kujiandaa mapema na amewaomba wakazi wa Bignona na Senegal kwa jumla kuacha kudharau kuhusiana na ugonjwa huo ambao unaua watu wengi zaidi kwa haraka na sasa ni tishio duniani.


Hivi karibuni kama mtakuwa mliona tulishiriki kama kampuni kwa ukaribu zaidi katika zoezi la kufikisha misaada kwa jamii.



 Kwanza tulianza kama Kampuni ya Global Publishers kupitia magazeti mawili ya Championi na Spoti Xtra na lengo kuu lilikuwa ni kuwafanya wanajamii ambao ni wasomaji wetu kujisikia wapo pamoja nasi.


Tunataka kushirikiana nao wakati wa raha lakini pia shida hasa kipindi hiki cha maambukizi ya ugonjwa wa Corona. Kila mmoja ana hofu na maisha yamebadilika, hivyo kushirikiana katika mapambano ni jambo sahihi zaidi.


Baadaye tuliendelea kutoa misaada kumuwakilisha nyota wa zamani wa Simba, Talib Hilal ambaye sasa anaishi nchini Oman akiwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Beach Soccer (soka la ufukweni). Yeye alivutiwa na kazi yetu ya kushirikiana na jamii katika kipindi hiki kigumu.


Talib ambaye pia amewahi kuwa kocha wa Simba na kuipa ubingwa, aliamua naye kutuma misaada yake nasi tukaifikisha kwa jamii kama alivyokusudia.


Uamuzi huu wa Talib ni mapenzi makubwa kwa jamii kwa kuwa yuko mbali sana na Tanzania lakini bado amekumbuka na kuona anaweza kusaidia.


Pamoja na kwamba uamuzi wake unajengwa na uungwana lakini unaweza kuwa funzo kwa wachezaji wengine au wanamichezo wote walio nje ya Tanzania lakini kiasili au wanatokea hapa Tanzania kwamba misaada yao inahitajika.


Ndiyo maana nilianza na Wague, kuonyesha kwamba ametoa misaada hata bila eneo alilolisaidia kuwa na mgonjwa hata mmoja, akiamini kuchukua tahadhari mapema ni vizuri zaidi.


Talib naye aliona tayari Tanzania imeanza kuathirika zaidi na Corona na wagonjwa wanaongezeka ndio maana akaanza na ndoo na sabuni, vitakasa mikono kwa lengo la kuchukua tahadhari na baadaye akatoa misaada ya chakula.


Talib na Wague ni wanamichezo ambao wanaona namna jamii ikiathirika kila kitu kinakuwa katika wakati mgumu kama unavyoona sasa michezo yote imesimama. Inasababisha kero na pia kuyumbisha kipato na kufanya maisha yawe magumu kabisa.


Hakuna ubishi lazima kuungana na kuunganisha nguvu zetu kupambana kwa nguvu kabisa na Corona ambayo si mzaha tena.


Kuunganisha nguvu ni pamoja na wenye nguvu zaidi au angalau kuwasaidia wasionacho katika sehemu ambayo tunaona inastahili. Ndio maana nasisitiza kwamba wachezaji au wanamichezo wanaocheza ligi mbalimbali za nje wana kila sababu ya kukumbuka nyumbani.


Binafsi sivutiwi sana na ukimya wao, naona kama wamelichukulia poa tatizo hili, naona kama wana nguvu ya kutoa msaada hata kama itakuwa kidogo lakini wameendelea kuwa kimya sana.


Nimeona watu wanaendelea kusema ukitoa misaada watu wasijue, hilo ni chaguo lakini hata kwenye dini inakubalika na hasa kama utakaposaidia na kuonyesha, lengo lako ni zuri kuwahamasisha na wengine wenye uwezo watoe basi hakuna tatizo.


Saidieni nyumbani, jitoleeni kusaidia mapambano dhidi ya Corona na jitokezeni kuwashika mkono wanaohitaji misaada kadiri ya uwezo wenu. Msiendelee kukaa kimya tu kama hamuoni kinachoendelea. 

SOMA NA HII  GUMZO LA UNUNUZI WA NEWASTLE NA KASHFA YA KIFO CHA MWANDISHI KASHOGGI