Home Uncategorized BILIONEA YANGA AFUNGUKA MKATABA WA YANGA NA LA LIGA

BILIONEA YANGA AFUNGUKA MKATABA WA YANGA NA LA LIGA

Mkurugenzi wa uwekezaji wa kampuni ya GSM inayoidhamini Yanga, Injinia Hersi Said amesema kuwa wataalam kutoka Ligi Kuu ya Hispania na klabu ya Sevilla tayari wameshaanza mchakato wa kuiongoza Yanga kuelekea katika mabadiliko ya kimfumo.

“Tayari wameanza hatua ya kwanza ambayo ni ukusanyaji wa data ili waweze kupata taarifa muhimu zitakazowasaidia katika suala hili,” alisema kiongozi huyo.

Katika hatua nyingine,  wachezaji tisa (9) wazawa watapunguzwa katika kikosi cha Yanga kwenye dirisha kubwa lijalo la usajili ili kupisha ujio wa nyota wapya.

Injinia Hersi Said, alisema kuwa uamuzi huo umetokana na mapendekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Luc Eymael.

“Kuna wachezaji kama tisa wazawa tunaweza kuachana nao na hawa ni wale ambao baadhi mikataba yao itakuwa imemalizika hivyo hatutowaongezea na wengine baadhi tutaangalia kama tutawatoa kwa mkopo au tunaachana nao vipi.

Kimsingi katika msimu ujao, benchi la ufundi limependekeza kikosi kiwe na wachezaji 26 ili kutoa nafasi kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi cha vijana kucheza upande wa timu ya wakubwa,” alisema Injinia Hersi.

Hersi ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya usajili ya Yanga na ile ya mabadiliko, aliliambia Mwanaspoti kuwa kipaumbele cha benchi la ufundi ni kuimarisha idara bya ushambuliaji.

“Changamoto kubwa ambayo imekuwa ikitukabili msimu huu ipo kwenye ufungaji hivyo kwa kiasi kikubwa usajili utalenga kuimarisha upande wa ushambuliaji lakini pia wachezaji wachache wa nafasi nyingine,” alisema Injinia Hersi.

Kiongozi huyo alifichua kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wapo mbioni kujiunga na timu hiyo ni beki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto ambaye wameshamalizana na klabu yake.

“Tumeshamalizana na Coastal Union juu ya mahitaji yao na wametupa ruhusa ya kufanya mazungumzo na mchezaji wao kama utaratibu ulivyo. Kwa sasa tunamngojea meneja wake ambaye yuko nje ya nchi,” alisema Injinia Hersi.

SOMA NA HII  ZAHERA AWAPA KIBANO ZESCO UNITED - VIDEO