Home Uncategorized EYMAEL AMPA MASHARTI MATATU MARRISON..LA SIVYO KUISIKIA YANGA KWENYE ‘BOMBA’

EYMAEL AMPA MASHARTI MATATU MARRISON..LA SIVYO KUISIKIA YANGA KWENYE ‘BOMBA’

Kocha wa Yanga Luc Eymael amesema kiungo wake kutoka Ghana, Bernard Morrison atarejea katika timu hiyo jijini Dar es Salaam, lakini kwa masharti matatu. Kuomba radhi wachezaji wenzake na benchi la ufundi, mashabiki na wanachama pamoja na viongozi na wadhamini wa Yanga.

Eymael amesisitiza kwamba Morrison pamoja na mchezaji yoyote wa Yanga lazima ajue kuwa, kila kitu anachokifanya ni kama timu huku akionya kuwa hakuna mchezaji nyota asiyepata msaada uwanjani kutoka kwa wenzake.

Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti jana, Eymael alisema Morrison akikamilisha masharti hayo ataunga na wenzake kujiandaa na mechi dhidi ya Azam FC.

Alisema kuwa amezungumza na mchezaji huyo kwa dakika 50 na kujua kosa lake ambalo anajutia huku akitanabaisha kwamba, baadhi ya mawakala wa soka wanatamaa ya fedha na kuwashawishi vibaya wachezaji.

Alisema kwa Morrison amegundua njama hizo na kukiri kukosea na ataomba radhi mbele ya wachezaji ili kujiandaa na mechi hiyo ambayo itatoa picha halisi katika vita ya kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara.

“Mimi sikuwepo, nimekutana mambo mengi ambayo si ya kawaida ndani ya klabu, kama kocha mkuu ni jukumu langu kutatua na kuiweka sawa timu.

Morisson ni moja ya tatizo hilo na hakuweza kusafiri kwenda Shinyanga, nilitaka kujua kuna tatizo gani, lakini muda haukutosha na kuamua kuondoka na Molinga (David),” alisema.

Aliongeza kuwa; “Niliongea na Morrison na kunieleza tatizo lake hadi kunizimia simu. Kuna baadhi ya mawakala wa soka wana matatizo na wana rubuni wachezaji, hata hivyo hilo ni kosa lake na anatakiwa kuomba radhi.”

Pia, amemtaka Morrison kutambua kuwa hakuna  mchezaji mkubwa kuliko timu na hakuna mchezaji nyota duniani anayecheza mpira peke yake uwanjani bila msaada wa wengine.

Alitolea mfano kuwa ; “Hata ukichukua akina Cristiano Ronaldo wawili, Messi wawili na Sergio Ramos wawili wacheze dhidi ya wachezaji 11, lazima watafungwa tu. Timu ni mchango wa watu wengi.”

“Najua kuwa Morrison kwa sasa ndiye mchezaji nyota wa Yanga, hilo halina ubishi, lakini lazima ajue umaarufu wake unatokana na msaada au ushirikiano na wenzake, hilo ni jambo muhimu kujua,  Yanga ni timu na wala si ya mchezaji mmoja pekee,” alisema.

SHANGWE BUNGENI

Jana wachezaji na viongozi wa Yanga walikaribishwa kwa shangwe katika ukumbi wa Bunge, Dodoma na kushangilia na wabunge.

Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye mara kadhaa amekuwa akiweka wazi mapenzi yake kwa Simba, alikiri kuwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga limebaki katika vichwa vya mashabiki.

Katika ukumbi huo, Spika alimtaka Morrison asimame asalimie wabunge lakini hakuwepo kutokana na kubaki Dar es Salaam.

Yanga itawavaa JKT Tanzania kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

SOMA NA HII  MAPROO WAWILI SIMBA KUKUTANA NA BALAA ZITO, KAGERE NDANI