Home Uncategorized KICHUYA ARUDI NA UTAMU WAKE

KICHUYA ARUDI NA UTAMU WAKE

WINGA wa Simba, Shiza Kichuya, ameanza kurejea katika utamu wake baada ya juzi kupiga soka la kiwango cha juu wakati timu hiyo ilipocheza na KMC mechi ya kirafiki Uwanja wa Mo Simba Arena.

Katika mchezo huo uliodhuriwa na mashabiki kibao, Kichuya alicheza winga ya kushoto, huku kulia akiwa, Luis Miquissone, kila mmoja akionesha vitu vyake.

Mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo, walishindwa kujizuia na kumshangilia, hususan alipokuwa akipiga krosi zake za ufundi ambazo walizikosa kwa muda mrefu.

Ikumbukwe kuwa tangu kichuya amerejea kikosini hapo kipindi cha usajili wa dirisha dogo, alikuwa hapati nafasi na kuwa mchezaji wa benchi.

Kichuya mwenyewe aliwahi kukiri sababu ya kukosa namba ni kutokana na kiwango chake kushuka baada ya kukaa nje muda mrefu alipokuwa nchini Misri, hivyo kuongezeka uzito.

Mchezaji huyo aliyejipatia umaarufu ndani ya Simba kutokana na kupiga mipira ya kona kiufundi, alitumia kipindi cha mapumziko ya janga la corona kujichimbia nyumbani kwao mkoani Morogoro akijifua vikali ili kupunguza uzito.

Mechi dhidi ya KMC imedhihirisha Kichuya amerudi kwa sababu alikuwa miongoni mwa wachezaji waliong’ara katika mechi hiyo.

Wachezaji wengine waliyoonesha vitu vyao ni Said Ndemla, aliyekuwa amesimama katikati na Jonas Mkude ambaye baadaye aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Ajib, aliyefunga bao la tatu kwa staili ya aina yake.

Kwa kiasi kikubwa wachezaji wote hususan wale wanaokaa benchi muda mwingi, walitumia michezo hiyo kuonesha kuwa wanarudi kivingine akiwamo, Gadiel Michael.

Akizungumzia michezo yote miwili, kocha msaidizi wa  Simba, Seleman Matola, alisema lengo lilikuwa kuwaona wachezaji baada ya kufanya mazoezi muda mrefu na wameridhishwa na kiwango.

“Hii michezo ilikuwa ya kirafiki sio kushindana kupata matokeo, kwa kweli wachezaji wetu wameonekana kupokea vizuri maelekezo ya benchi la ufundi, naamini tutarudi uwanjani tukiwa fiti.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA JUMANNE