Home Uncategorized KISA CORONA…SHIBOUB ASUBIRI RUHUSA YA RAIS SUDANI KURUDI TZ..!!

KISA CORONA…SHIBOUB ASUBIRI RUHUSA YA RAIS SUDANI KURUDI TZ..!!

NYOTA wa Simba, Sharaf Shiboub, anasubiri huruma ya Serikali ya Sudan ili kurejea Tanzania kuendelea na majukumu yake katika kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Shiboub kwa sasa yupo nchini kwao Sudan baada ya Serikali ya Tanzania kusimamisha shughuli za michezo Machi 17, mwaka huu kutokana na hofu ya kuenea kwa maambukizi ya virus vya corona.

Japo kwa sasa shughuli za michezo zimeruhusiwa hapa nchini, lakini kwa Sudan bado hakuna ruhusu ya kutoka au kuingia kutokana na janga hilo la corona.

Kutokana na hali hiyo, Shiboub amekwama huko, akisubiri iwapo Waziri Mkuu wa Sudan ambaye ndiye kiongozi mkuu wa Serikali ya nchi hiyo, Abdalla Hamdok, atafungua mipaka.

Katika kikosi cha Simba, tayari nyota wote wa kimataifa wamewasili Tanzania, wakiwamo Meddie Kagere (Rwanda), Francis Kahata (Kenya), Clautos Chama (Zambai) na Luis Miquissone (Msumbiji), akikosekana Shiboub pekee.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, ameliambia BINGWA jana kuwa kuna ugumu wa kumpata Shiboub kutokana na mazingira yalivyo nchini kwao.

“Shiboub yupo kwenye nchi ambayo imekuwa na sheria ngumu na mipaka imefungwa kutokana na janga la corona, hivyo ni ngumu kwake kuweza kurejea kwa wakati.

“Tumejaribu kuwasiliana na Serikali ya Sudan kama tulivyofanya kwa wenzake, lakini kumeonekana bado kuna ugumu, hivyo tunasubiri hadi waondoe zuio la kutoka (lockdown) ndipo arejee, lakini kutokuwepo kwake, hakutazuia timu kupata kile tunachohitaji,” alisema.

Rweyemamu alisema kuwa Simba ina wachezaji wengi, hivyo watapata ushindi katika mechi zao na kuchukua taji la ubingwa ambalo wana hamu ya kulitwaa kwa mara ya tatu mfululizo.

Shiboub amesajiliwa na Simba msimu huu kwa kandarasi ya mwaka mmoja, akiwa ameifungia timu hiyo mabao mawili na kutoa pasi sita za mabao.

SOMA NA HII  SIMBA YAWEKA MEZANI MILIONI 10 KWA AJILI YA KELVIN YONDAN, METACHA MNATA, JUMA KASEJA