Home Uncategorized MOLINGA AWAJIA JUU YANGA

MOLINGA AWAJIA JUU YANGA

MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, raia wa DR Congo, David Molinga, amewajia juu baadhi ya watu ndani ya klabu hiyo wanaomhusisha mara kwa mara na matendo mabaya.

Akizungumza na BINGWA jana, Molinga anadaiwa kugoma kwenda Shinyanga kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mwadui utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Kambarage, hata hivyo anashangazwa kuona kila jambo baya linalosemwa ndani ya klabu hiyo, lazima atahusishwe.

Kabla ya wachezaji wa Yanga kuondoka alfajiri jana, uongozi wa klabu hiyo kupitia kwa ofisa habari wake, Hassan Bumbuli, alitoa orodha ya nyota 22 watakaosafiri  kwenda Shinyanga wakiwamo Molinga, lakini waliopanda basi ni 19, huku wengine wakibaki jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Yanga, Molinga ni miongoni mwa wachezaji waliobaki, huku ikielezwa alimwambia meneja wa timu hiyo, Abeid Mziba, haoni sababu ya kocha kuwajumuisha Bernard Morrison na Haruna Niyonzima ambao hawakufanya mazoezi na timu na wakisafiri hatakwenda Shinyanga.

Hata hivyo Molinga alikanusha madai hayo huku akisema amekuja Tanzania kucheza mpira  na tangu timu ilipoanza mazoezi ameshiriki kikamilifu inakuwaje leo agome kwenda Shinyanga.

“Jana listi ilitoka na mimi jina langu hajakwepo sasa itasemekana vipi mimi nimegoma? kama ndio hivyo muulizeni kocha ndio alitajia listi yake, nachukizwa na kuona mara kwa mara kila kitu mimi tu, hata kama sijafanya kitu kibaya utasikia tu Molinga ‘This is too much.”

Molinga aliongeza:  “Molinga atapita Yanga itabaki, hakuna haja ya kuchafuliana majina, tusubiri miezi miwili iishe ili tumalizane, kila mtu atapita tu Yanga.”

Kikosi cha wachezaji 19 cha Yanga kilichokwenda Shinyanga ni Farouk Shikhalo, Paul Godfrey, Juma Abdul, Adeyum Saleh, Jaffary Mohamed, Kelvin Yondani, Lamine Moro na Said  Makapu.

Wengine ni Abdulaziz Makame, Feisal Salum  Abdallah ‘Fei Toto,  Mapinduzi Balama, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa, Deus Kaseke na Patrick Sibomana, Yikpe Gnamien, Ditram Nchimbi na Tariq Seif.

SOMA NA HII  YANGA KUMLETA CHID BENZ VS MADEAMA