Home Uncategorized STAILI MPYA SIMBA YA KUKABA SI MCHEZO

STAILI MPYA SIMBA YA KUKABA SI MCHEZO

KWA mara ya kwanza jana Simba imeonyesha kwamba wao ni levo nyingine kabisa baada ya kucheza mechi mbili asubuhi na jioni na kupiga mabao 7.

Lakini Kocha Sven Vandenbroeck aliibuka na staili mpya ya matumizi ya mabeki wake ambao mashabiki wa timu hiyo waliimisi na kuwafanya wafurahie kwelikweli na kulala wakiwa raha mustarehe.

Katika mechi ya kirafiki ya kwanza ambayo ilipigwa jana asubuhi Simba walishinda mabao 4-2 timu ya Transit Camp ya Daraja la Kwanza kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena mashabiki waliona vitu vipya na jioni KMC akala mabao 3-1 na kikosi tofauti kabisa.

Sven alianza na mabeki wa kati watatu ambao ni Yusuph Mlipili, Tairone Santos na Erasto Nyoni, mfumo ambao mara ya mwisho kuutumia ilikuwa ni misimu miwili iliyopita.

Misimu miwili iliyopita Simba walicheza na mabeki watatu wa kati ikiwa chini ya kocha, Mfaransa Pierre Lechante ambaye alikuwa akiwatumia Mganda Juuko Murshid, Mghana James Kotei na Mlipili.

Simba baada ya kuanza na mabeki watatu wa kati jana, Sven aliwataka Shomary Kapombe kulia na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kushoto kucheza kama walinzi-mawinga.

Wakati huo Rashid Juma na Deo Kanda, ambao kiasili ni mawinga, walicheza eneo la katikati nyuma ya washambuliaji wawili ambao walikuwa Meddie Kagere na Mzamiru Yassin.

Kiungo mmoja wa kati ambaye alikuwa Gerson Fraga jukumu lake linakuwa kulinda safu ya ulinzi ambayo ilibaki na mabeki watatu na muda mwingine kuongeza nguvu katika kushambulia ambapo wanakuwa wachezaji watano kwenye eneo la timu pinzani.

Mbinu hiyo ilionekana kuwasaidia Simba kwani walimiliki mpira muda mwingi kwa maana ya kupasiana pasi ndefu na fupi kama ambavyo Sven alikuwa anahitaji. Walizuia mashambulizi ya Transit kwani muda ambao wanashambulia wanakuwa wachezaji sita mpaka saba lakini muda ambao wanashambuliwa wanakuwa idadi hiyo hiyo.

Mfumo huo ambao Sven aliwapatia ni (3-5-2), Simba walianza kutumia msimu wa 2017-18 na ukawapa mafanikio ya kutwaa ubingwa wa ligi chini ya Lechantre.

Sven alieleza kwa ufupi; “Hiki ambacho unakiona katika mazoezi yetu ndio tunakwenda kukitumia na kukifanya katika mechi zetu za kimashindano, ndio maana tumetaka kucheza mechi ya usiri ila kutokana uwanja wetu hauna uzio ndio mmepata nafasi ya kuja kushuhudia.”

Kipa chaguo la kwanza katika kikosi cha Simba, Aishi Manula alisema; “Tunaangalia upungufu na ubora wa timu yetu ili kwenda kuyarekebisha makosa na kufanya vizuri katika michezo ya kimashindano.”

DHIDI YA TRANSIT

Katika ushindi huu mabao yote ya Simba yalifungwa na wachezaji wa kigeni Wabrazili Gerson Fraga, Tairone Santos, Mnyarwanda Meddie Kagere na Mkongomani Deo Kanda. Transit walitupia Hamad Habib na Nisile Kisimba.

KMC WAKALA 3

Hapa ndipo Jonas Mkude alipoumia jioni na kukimbizwa hospitali na gari la wagonjwa (Ambulance). Kiungo huyo alionekana akilalamikia maumivu ya bega baada ya kugongana na mchezaji mmoja wa KMC wakati wakiwania mpira katika mchezo huo wenye ushindani mkubwa.

Kwa mujibu wa daktari wa Simba, Yassin Gembe, Mkude ameumia vidole vya mguu wa kulia wakati akiwania mpira jambo lililomlazimisha mwamuzi Said Pambalelo kusimamisha mpira ili kuruhusu apewe huduma ya kwanza.

Madaktari wa Simba waliingia uwanjani na kumpa huduma ya kwanza kisha kumbeba hadi nje ya uwanja ambapo waliendelea kumpa matibabu huku Mkude akionekana kugugumia kwa maumivu.

Baada ya dakika takribani tano kupita ndipo madaktari wakaita gari la wagonjwa lililokuwepo uwanjani hapo na kumchukua mchezaji huyo na kumuwahisha hospitali.

Mabao ya Simba kwenye mechi ya jana yalifungwa na John Bocco (mawili) na Ibrahim Ajib. Bao la KMC lilifungwa na Charles Ilamfya.

KIKOSI CHA JIONI

Aishi Manula, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Paschal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Said Ndemla, John Bocco, Luis Miquisonne na Shiza Kichuya

CHA ASUBUHI

Benno Kakolanya, Shomary Kapombe, Mohammed Hussien ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Yusuph Mlipili, Tairone Santos, Rashid, Gerson Fraga, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere na Deo Kanda.

CHAMA AMERUDI HUKO

Kiungo wa Mzambia Clatous Chama alitumia muda kujifua peke yake chini ya kocha wa viungo Adel Zrane ambaye alikuwa akimfuatilia kwa karibu.

SOMA NA HII  NAMUNGO KAMILI GADO KUVAA MBEYA CITY LEO SOKOINE