Home Uncategorized TFF KUWAKABIDHI SIMBA KOMBE LAO KWA UTARATIBU HUU..!!!

TFF KUWAKABIDHI SIMBA KOMBE LAO KWA UTARATIBU HUU..!!!

KAMA Simba wakishinda mechi yao Jumamosi hii dhidi ya Prisons, watakuwa wamebeba rasmi ubingwa kwa maranyingine.

Lakini licha ya kusaliwa na mechi kadhaa mkononi, Bodi ya Ligi imesema kama wakiomba wapelekewe kombe lao kabla ya msimu kumalizika watawawekea utaratibu.

Simba ikitetea ubingwa huo kesho, itakuwa ni mara ya tatu mfululizo kulibeba kombe hilo katika misimu ya hivi karibuni wakianza msimu wa 2017-18.

Vinara hao wamecheza michezo 32, na kufikisha pointi 78 huku wakisaliwa na pointi tatu tu kumaliza kazi bila kuangalia matokeo ya timu yoyote.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania(TPLB), Steven Mnguto alisema kwa utaratibu ambao wamejiwekea hawatawapelekea Simba kombe katika Uwanja wa Sokoine Mbeya Jumamosi hata kama watashinda.

Alisema utaratibu wao ambao wamejipangia kuwa wanataka kuwakabidhi mabingwa kombe pamoja na sherehe zote katika mechi yao ya mwisho lakini kama watataka vinginevyo wapeleke maombi rasmi.

β€œKama kuna mechi ambayo wanataka wakabidhiwe ubingwa wao watatuletea maombi hayo lakini kwetu tulipanga kuwapa kombe pamoja na sherehe kiujumla katika mechi ya mwisho,” alisema Mnguto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Coastal Union ya Tanga.

Kwa upande wa Simba kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa alisema; β€œTutakutana viongozi na tutafanya kikao cha ndani ambacho ndio kitatoka na majibu kwamba tunaweza kusubiri hadi mechi ya mwisho ndio tukabidhiwe kombe pamoja na kufanya sherehe za ubingwa au tufanye maombi ya kuchukua katika mechi fulani.”

SOMA NA HII  WINGA MPYA WA YANGA KUANZA MAJUKUMU YAKE