KOCHA Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa, amesema kuwa katika mazoezi ya siku tano ambayo wachezaji wamefanya, amebaini kuna nyota wao watano walioongezeka uzito jambo lililosababisha awape programu tofauti na wengine.
Mkwassa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na vyombo vya habari kabla ya kuanza kwa mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Dar es Salaam, kujiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Timu ya Halmashauri ya Kinondoni (KMC) kesho Uwanja wa Taifa, jijini.
Mkwasa alisema sababu kubwa ya wachezaji hao kuongezeka uzito ni kushindwa kujipangilia aina ya vyakula walivyokuwa wakitumia pamoja na kutofanya mazoezi kipindi cha mapumziko ya janga la corona.
“Kuna wachezaji wameongezeka uzito na kushindwa kuendana na aina ya mazoezi ninayotoa, nimelazimika kuwapa programu ya pekee yao na kuwapangia aina ya vyakula vitakavyowapunguza uzito.
“Kwa programu nilizowapa, hadi wiki ijayo watakuwa vizuri na kuungana na wenzao katika mazoezi kwaajili ya mechi yetu ya Mwadui,” alisema.
Akizungumzi mechi yao na KMC kesho, Mkwassa alisema itakuwa ngumu kwao kwa sababu wenzao wameanza mazoezi mapema tofauti na wachezaji wake.
“Itakuwa mechi ngumu sana kwetu, kwa sababu wenzetu wameanza mazoezi mapema tofauti na sisi, lakini pia tatizo la uzito liliopo kwa baadhi ya wachezaji wangu.
“Lakini nafurahi kuona tutapata changamoto itakayotupa mwanga wa kitu gani cha kufanya kabla ya mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC,” alisema.
Alisema mara baada ya mechi na KMC, wachezaji wataingia kambini huku safari ya kuelekea mkoani Shinyanga ikiwa ikipangwa kuwa katikati ya wiki ijayo.