Home Uncategorized GWAMBINA HUKU JUU KUNA ISHU YA KUSHUKA PIA, MIPANGO MUHIMU

GWAMBINA HUKU JUU KUNA ISHU YA KUSHUKA PIA, MIPANGO MUHIMU


USHINDANI mkubwa unaonekana kwenye timu ambazo zinapambana kusaka nafasi ya kushiriki Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2020/21 ndani ya Ligi Daraja la Kwanza, hili ni jambo jema na linafurahisha.

Tunaona kwamba kwenye kundi B habari ya mshindi wa kundi imeshaisha na kuzimwa jumla na Gwambina FC ambao wao tayari wana tiketi yao mkononi kwa ajili ya msimu ujao ndani ya Ligi Kuu Bara.
Hawa Gwambina ninawapa tano kwa kuwa hesabu zao tangu mapema zilikuwa wazi na walionyesha kwamba wamedhamiria kile ambacho wanakitafuta na wakakipata kwa kuwa walikuwa na nia.
Anza kutazama uwekezaji wao kwa namna ambavyo walikuwa wanafanya, hawajabahatisha wala kupendelewa bali walikuwa na kitu ambacho wanakiona mbele wakaanza kukifanya mapema.
Wakati wanaanza wengi walidhani wamekuja kufanya mauzo kumbe wamekuja kufanya kazikazi kwelikweli na wamepanda huku wale waliokuwa wakiwabeza wanabaki wakiwashangaa.
Kuonyesha kwamba wamedhamiria kufanya kweli walianza kuwekeza kwenye upande wa miundombinu jambo ambalo lilikuwa haliwapi taabu wao wakihitaji kufanya mazoezi muda wote wanafanya.
Gwambina Complex ni mfano wa uwanja mzuri ambao kila timu zinapaswa ziutazame kuwa ni mfano na zifikirie namna ya kuweza kufikia hatua kama ile kwa kufanya uwekezaji mkubwa na unaolipa.
Mbali na uwanja pia kwenye upande wa falsafa za wachezaji wamekuwa na nia moja ndani ya uwanja kwa kucheza kwa moyo wote unaona tangu mchezo unaanza mpaka unakamilika wana kasi ileile.
Fikiria mchezo wao wa mwisho ambao uliwapa tiketi ya kushiriki ndani ya ligi mbele ya Pamba , Uwanja wa CCM Kirumba ulipigwa mpira mwingi mwanzo mwisho.
Ili kujua kwamba walikuwa na jambo lao tangu zamani wamekuja kupata ushindi muda ambao hakuna aliyekuwa akifikiria kwamba watashinda dakika za lala salama watu wanaingia kambani mpira unawekwa kati.
Hili liwe somo kwa timu nyingine ambazo zinajipanga kupanda ligi msimu unaofuata hata wale ambao bado wanapambana kutafuta nafasi ya kushiriki ndani ya ligi lazima wawe makini katika kutimiza malengo ambayo wamejiwekea.
Tazama namna ambavyo walikuwa wamewekeza kwa wachezaji namna ambavyo wanajituma ndani ya uwanja na kukubali kwamba kushindwa mwanzo sio mwisho wa mchezo.
Hilo walithibitisha Uwanja wa Uhuru wakati wanapambana na Transit Camp baada ya kuwa nyuma kwa bao 1-0 ila mwisho wa dakika 90 ngoma inakamilika 1-1 huu ni ushindani mkubwa na unatakiwa kuwa kwenye mioyo ya wachezaji wote.
Achana na hilo tuje kwa upande wa nahodha wao ambaye amekuwa ni mhimili mkubwa kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi anaitwa Jacob Massawe, amekuwa na mchango mkubwa ndani ya timu.
Ndivyo inavyotakiwa kwa wachezaji wote kutimiza majukumu kwa wakati na kuendelea kutoa ushirikiano kwa wachezaji wengine ili kufikia malengo ya timu.
Uzoefu wake wa kucheza kwenye ligi pamoja na mechi nyingi za ushindani umemfanya amezidi kuwa bora. Wachezaji pamoja na benchi la ufundi wote wanajivunia uwepo wake ni jambo la msingi kutambua mchango wa mchezaji na nafasi yake katika kuwaunganisha wachezaji na mashabiki kwenye furaha.
Kibindoni akiwa na mabao yake 10 ni namba moja kwa utupiaji ndani ya Gwambina ila bado amekuwa ni chachu ya ushindi kwa wenzake katika hili wachezaji wanapaswa kujifunza kwamba uongozi ni kuwajibika na kushirikiana na wengine bila kuchoka.
Sasa Gwambina mmepanda ligi sawa, lakini mnapaswa muangalie namna gani mnaweza kuwa na maisha marefu ndani ya ligi ambayo ushindani wake sio wa kuzembea kwani huku ukizubaa unakwenda na maji.
Tunaona kwamba kwa sasa bado mna mechi mbili mkononi lakini mshapanda hivyo katika hilo mnapaswa kupewa hongera lakini lazima mtambue kwamba kuna kitu kinaitwa kushuka daraja.
Kwa sasa kwenye ligi yamebaki makundi matatu baada ya lile la kwanza la bingwa kuisha, sasa ni vita ya 10 bora, play off na kushuka daraja hapo ndipo unaona namna gani huku juu mambo yalivyo.
Nina amini kwamba makocha ambao wapo wanatambua kuhusu maisha ya ligi, Athuman Bilal anajua namna ushindani ulivyo hivyo itakuwa vizuri akianza kuwaibia namna mambo huku yalivyo.
Kwa sasa ni lazima mipango ianze kwa kasi kwani hakuna muda wa kupumzika kwenye maisha ya soka mwanzo mwisho hesabu na kuangalia ramani upya za kuweza kufanya vizuri.
Kama ambavyo mmeweza kufanya ndani ya Ligi Daraja la Kwanza kwa kucheza mechi nyingi na kupata matokeo basi na huku ndani ya ligi kinachohitajika ni matokeo.
Msije huku kufanya mafunzo kwa muda kama ilivyokuwa kwa Njombe Mji hapana tunahitaji kuona mnakuja na mnaleta ushindani kama ilivyo kwa JKT Tanzania ambayo kwa sasa ni msimu wake wa pili ila bado ina uhakika wa kubaki kwenye ligi.
SOMA NA HII  MTUPIAJI HUYU AKUBALI KUTUA YANGA