Home Uncategorized KIUNGO WA YANGA ISHU YAKE YA KUTUA SIMBA YALETA MPASUKO

KIUNGO WA YANGA ISHU YAKE YA KUTUA SIMBA YALETA MPASUKO


BENCHI la Ufundi la Simba chini ya Kocha Mkuu Mbelgiji, Sven Vandenbroeck limejigawa katika usajili wa kiungo mshambuliaji wa Yanga Mghana, Bernard Morrison.

Mghana huyo hivi sasa anatajwa kujiunga na Simba huku tetesi zikienea huenda akajiunga na timu hiyo kwenye msimu ujao baada ya kuwepo mazungumzo ya siri.

Kiungo huyo hivi karibuni aliingia kwenye mzozo mkubwa na mabosi wa timu yake baada ya kukanusha kutoongeza mkataba wa miaka miwili tofauti na ule wa awali wa miezi sita aliousaini Januari, mwaka huu.

Taarifa zinaeleza kuwa licha ya uongozi wa Simba kuhitaji saini ya Mghana, lakini baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi wameonekana kutomuhitaji staa huyo wa Yanga.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa viongozi hao wa ufundi wameingia hofu ya kuja kuivuruga timu mara baada ya kujiunga Simba kwa yale matukio ya kiutovu ya nidhamu ambayo anaendelea kuyafanya kwenye timu yake ya Yanga.

Aliongeza kuwa kama uongozi unahitaji mchezaji wa aina ya Morrison, wapo wengi hivyo ni vema uongozi ungewaleta kutoka kwenye nchi za Afrika Magharibi lakini siyo kumleta Mghana huyo.

“Morrison ni kati ya viungo bora hivi sasa katika ligi ya hapa nyumbani, tatizo lake ni utovu wa nidhamu kama ameweza kufanya matukio ya ajabu akiwa Yanga atashindwa hapa Simba.
“Ni vema viongozi wakaliangalia hilo, kwani kama wakihitaji mchezaji wa aina ya Morrison wapo wengi Afrika Magharibi, kikubwa watafute watu wa kufanya ‘scouting’ wazuri watakaoleta mchezaji wa aina yake.
“Kwani nina hofu kubwa kama akija hapa atatuvuruga, hivyo kwa tahadhari nashauri viongozi waachane naye watafute mchezaji mwingine wa aina yake ili asituvuruge hapo baadaye,” alisema mtoa taarifa huyo.
Kiungo huyo hivi karibuni alisema kuwa hivi sasa yeye ni mchezaji huru kwani mkataba wake wa miezi sita umemalizika Jumanne ya wiki hii, hivyo ameomba aondoke Yanga na kwenda kwingine alikopanga kwenda.

Chanzo: Championi
SOMA NA HII  JESHI LA DODOMA FC LEO DHIDI YA YANGA,SHEIKH AMRI ABEID