Home Uncategorized MUUAJI WA SIMBA AREJEA KWA KISHINDO, BALAA LAKE LAMFANYA KOCHA ATABASAMU

MUUAJI WA SIMBA AREJEA KWA KISHINDO, BALAA LAKE LAMFANYA KOCHA ATABASAMU


BERNARD Morrison, kiungo mshambuliaji ndani ya Klabu ya Yanga amerejea na makali yake yaleyale ya siku zote jambo ambalo limempa tabasamu Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael. 

Morrison alikuwa kwenye mvutano na uongozi wa Yanga kuhusu ishu ya mkataba ambapo yeye alikuwa anadai kuwa ana dili la miezi sita huku uongozi ukiweka wazi kuwa ana dili la miaka miwili.

Shauri hilo lilipelekwa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) ambao waliweka wazi kuwa Morrison ni mchezaji halali wa Yanga na anapaswa aendelee kuitumikia Klabu hiyo kwa kuwa ana mkataba nayo.

Hakuwa sehemu ya kikosi kilichomenyana na Biashara United Uwanja wa Karume, kwenye sare ya bila kufungana Julai 5, kuumia kwa Haruna Niyonzima na umuhimu wa mechi dhidi ya Simba, Julai 12 kulimfanya Eymael awaambie viongozi wa Yanga wampe tiketi Morrison akamalizane na Kagera Sugar. 

Jana, Julai 8, kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar, Morrison alifunga bao pekee la ushindi dakika ya 78 na kuifanya Yanga kusepa na pointi tatu muhimu baada ya dakika 90 kukamilika kwa ushindi wa bao 1-0.

Eymael amesema kuwa alitumia muda mwingi kuongea na Morrison jambo ambalo limempa matumaini katika mechi ambazo zimebaki.

“Nimeongea na Morrison muda mrefu na kujua kwamba kuna mambo ambayo yapo kwenye kichwa chake, mengine sina uwezo wa kuyazungumzia kwa kuwa yatazungumzwa na viongozi.

“Kwangu mimi alichoniambia ni kwamba yupo tayari kucheza na nina amini yupo tayari kwani ni mchezaji wa Yanga,” amesema.

Machi 8, Morrison alimtungua Aishi Manula wakati Yanga ikishinda bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, ana jumla ya mabao matano ambapo manne amefunga kwenye ligi na moja kwenye Kombe la Shirikisho.

SOMA NA HII  FAROUK SHIKALO AZUNGUMZIA HATMA YAKE NDANI YA YANGA