Home Uncategorized NAWAKUMBUSHA TU KUWA KUNA MAISHA BAADA YA SIMBA VS YANGA

NAWAKUMBUSHA TU KUWA KUNA MAISHA BAADA YA SIMBA VS YANGA






NA SALEH ALLY
USIJALI nani alionekana bora au kushinda au kupoteza baada ya mechi ya jana ya watani Simba na Yanga.

Unajua namna kulivyokuwa na tambo kabla ya mechi hiyo ya jana ya Kombe la Shirikisho ya Azam Sports kati ya watani hao na kila upande ulikuwa unajiamini.

Baada ya Yanga kufanya vizuri zaidi katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba na kubeba pointi nne kati ya sita huku Simba wakibeba moja tu, walionekana kujiamini kupita kiasi na walikuwa na haki ya kufanya hivyo kwa kuwa rekodi ya hivi karibuni inaonyesha wao ni bora zaidi ya watani wao.

Watani wao walikuwa wanaamini kwa takwimu, kweli ni sahihi kwamba wao wana kikosi bora zaidi ya Yanga. Lakini walishindwa kulidhibitisha katika mechi hizo ambazo ya kwanza iliisha kwa sare ya mabao 2-2 baada ya Yanga kusawazisha mara mbili na ya pili, Simba wakalala kwa bao 1-0 na Yanga wakatandaza soka safi la kitabuni. 

Hakuna ubishi tena kwamba kila baada ya mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba, maisha huwa yanaendelea kama kawaida. Maisha huwa yanakuwa na nafasi nyingine ya kujaribu mambo mengine na kunakuwa na nafasi nyingine ya Yanga na Simba kukutana.

Mfano mzuri, Simba na Yanga wamekutana mara tatu katika msimu mmoja. Mechi mbili za ligi kuu na moja ya Kombe la Shirikisho, kama burudani ya Kariakoo Dabi imekuwa ni ya kutosha kwa msimu huu na ndani ya mwaka mmoja tu wamekutana mara tatu na kuna nafasi ya kukutana mara nyingine, huenda katika ligi miezi ya mwisho ya mwaka huu.
Nasisitiza sana suala la kwamba kuna maisha baada ya Simba na Yanga kwa kuwa kila baada ya mechi hii, wako wanapoteza kazi zao, wako wanajengewa chuki, wako wanaonekana ni wasaliti wako wanahisiwa kadha wa kadha na wako wanaolalamikiwa au kulaumiwa kupindukia.

Mchezo kama huu, kwa kuwa macho na masikio ya wengi yanaelekezwa kuna haja ya kujifunza na kukubali kuwa mechi hiyo ni kama nyingine za Ligi Kuu Bara lakini hii inakuwa gumzo kutokana na historia. Lakini haizuii kuwa mechi ya soka na ambayo baada ya hiyo nyingine zinafuatia au maisha yanaendelea.

Utaona hakuna timu ambayo hukubali kufungwa bila ya kumtafuta mchawi. Anaweza kuwa mchezaji, anaweza kuwa kiongozi au mwamuzi, anaweza kuwa yeyote yaani ilimradi watu hutengeneza kituo cha kushushia hasira zao baada ya kupoteza mchezo au kushindwa kushinda.

Kama unakwenda katika mechi, kitakachotokea lazima kiendane na sare, kushinda au kufungwa na bahati nzuri kila anayekwenda uwanjani au kufuatilia mchezo anajua kabisa kati ya hayo matatu yatatokea na sababu za kutokea tunajua sote, lazima iwe kosa au makosa ya mchezaji au wachezaji.

Bila makosa, hakuna timu ingekuwa inashinda dhidi ya mwenzake na kama ni makosa lazima wawe wale wanaocheza mule ndani, kuanzia wachezaji hadi waamuzi. Hata uzuie vipi, ili moja ifunge lazima kuwe na kosa au makosa.

Sasa malumbano yanayopelekea wengine kuwachukia wengine, wengine kufukuzwa kazi au kuonekana kama ni maadui, ni mambo yaliyopitwa na wakati na yanayoonyesha namna ushabiki ulivyotumeza badala ya furaha yenyewe ya mpira na kuamini suala la maisha kuendelea baada ya mechi kama hiyo ya jana.

Simba na Yanga ni mchezo, hauwezi kuwa zaidi ya maisha ya kila siku. Mechi ikipita, acha liwe gumzo na burudani lakini chuki za kipuuzi, watu kuamini kashfa na matumizi ndio hoja, ni kupungukiwa uwezo wa kufikiri kwa usahihi. Tuanzie leo kubadilika na kuamini, mechi imepita jana, leo ni maisha mapya.
SOMA NA HII  CAF YAMPA TANO MRITHI WA SENZO SIMBA