Home Uncategorized USHINDANI NDANI YA LIGI KUU BARA UNAHITAJIKA, TIMU ZIBORESHE VIKOSI MSIMU UJAO

USHINDANI NDANI YA LIGI KUU BARA UNAHITAJIKA, TIMU ZIBORESHE VIKOSI MSIMU UJAO


VITA kubwa kwa sasa ambayo imebaki kwenye Ligi Kuu Bara ni suala la kugombania nafasi ya pili kwa timu zilizo ndani ya tano bora huku zile nyingine zilizo chini ya hapo nazo zina jambo lao linasaka.
Ipo wazi kwa sasa timu 10 hazina uhakika wa kubaki ndani ya Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao kutokana na kuwa na pointi ambazo zinafuatana kwa ukaribu na mchezo ambayo inafanana jambo ambalo linafanya kila mmoja awe na hesabu zake.
Hebu tuache kwanza hilo tuje na hawa wanaogombania nafasi ya pili kwa sasa ambao ni Yanga na Azam FC kwa sasa kuna jambo la kutazama wapi ambapo walikwama awali wakati ligi inaanza.
Tuache zile sababu za kuyeyusha pointi kadhaa kwa timu kwa kueleza kuwa waamuzi waliboronga ama AC ziliwashwa hayo tuweke pembeni tuje na hoja kidogo ambazo zinaweza kufanyiwa kazi.
Kama ikiwa kwa upande wa waamuzi hata Simba ambao ni mabingwa nao wamenyooshwa pia hebu jikumbushe kidogo wakati Simba inashinda mabao 2-0 mbele ya Coastal Union, bao la Meddie Kagere lililofutwa ilikuajekuaje, achana na hilo rudi wakati Simba inaonja joto ya jiwe kwa kufungwa bao 1-0 na JKT Tanzania.
Kuna bao moja lilifungwa na Gerson Fraga ikapigwa chini kwa madai kuwa alikuwa ameotea. Kwa Yanga pia nao wamepitia msoto kama huo mabao yao yamekutana na rugu na Azam pia wana maumivu hayo hivyo wote ni watoto wa baba mmoja kwenye maumivu.
Hapa tuzungumzie ule ukweli katika kuboresha soka letu wakati ujao ni namna gani msimu ujao unaweza kuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa mpaka sasa hakuna ambaye ameweza kuonyesha ule ushindani wa kweli.
Ndio ninasema hivyo kwa sababu timu inayoshika nafasi ya kwanza inaongoza katika kila kitu, hii ni hatari na inaleta picha kwamba iwapo hakutakuwa na maboresho kwa timu zetu msimu ujao pia zitaanza kugombania nafasi ya pili ambayo haina taji zaidi ya heshima.
Ukianza na mtupiaji namba moja anatoka Simba, Meddie Kagere ana mabao 19,mtengeneza mipango namba moja anatoka Simba, Clatous Chama ana pasi nane, timu iliyofungwa mabao machache ni Simba imefungwa mabao 16, timu yenye sare chache ni Simba ina sare tatu.
Hapa ndipo ambapo ujanja wa Simba ulipo hivyo Yanga ambao kinara wao ni David Molinga kwa utupiaji akiwa na mabao 10 huku wa kutengeneza pasi akiwa ni Juma Abdul mwenye pasi sita hizi ndizo sehemu za kufanyia maboresho ili kuweza kuleta ushindani mkubwa msimu ujao.
Ukitazama Yanga, inaonekana kwa kiasi fulani kuondoka kwa Ibrahim Ajibu bado hakujapata jibu lake kwani mpaka sasa hakuna mtengeneza mipango ambaye amefikia nusu ya rekodi yake aliyoweka msimu uliopita wakati akifunga mabao saba na kutoa pasi 17. Kuna umuhimu wa kufanyia kazi hili ili upate ushindi ni lazima ufunge.
Azam FC huwa wanaanza vizuri mwanzo ila katikati huwa wanasahau walikotoka. Bado kuna tatizo la ufungaji ndani ya Azam FC msimu uliopita kinara alikuwa ni Donald Ngoma alifunga mabao 10 mpaka anapigwa chini alikuwa amefunga mabao matatu na kwa sasa kinara wao ni Obrey Chirwa mwenye mabao nane huku mtengeneza mipango akiwa ni Nicolas Wadada mwenye pasi saba.
Kwa timu hizi wakati zinapambana kutafuta nafasi ya pili zijipange pia kutafuta wachezaji ambao watakuwa wanawapa matokeo ndani ya dakika 90 ili bingwa awe anapatikana mwishoni na sio anabaki na mechi mkononi ushindani unapotea.
Kwa zile ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja ni wakati wa kupambania kombe kwa sasa waamuzi nyie kazi yenu iwe moja tu kusimamia sheria 17 inatosha mengine waachieni wachezaji.
SOMA NA HII  MZUNGU WA YANGA ATOA SOMO HILI BONGO