Home Uncategorized WAAMUZI HAKUNA HAJA YA KUPEPESA MACHO, WACHEZAJI KAZI MOJA KUPAMBANA

WAAMUZI HAKUNA HAJA YA KUPEPESA MACHO, WACHEZAJI KAZI MOJA KUPAMBANA

 


KIVUMBI kinazidi kuwaka kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo kwa msimu huu mpya wa 2020/21 unaoyesha kwamba sio wa kitoto.

Ni Septemba 6 mwaka huu 2020 mambo yalianza ambapo tulishuhudia mzunguko wa kwanza wenye ushindani wake mfano wake hakuna.

Yote yameweza kutokea kutokana na timu zote kupata muda wa kujipanga na hasa kuanzia kwenye usajili mpaka maandalizi ya mwisho licha ya kuwa na muda mfupi wa kufanya hivyo.

Hii yote ilitokana na janga la Virusi vya Corona ambalo liliivuruga dunia na bado kwa sasa linasumbua kwa wenzetu ikiwa ni pamoja na Kenya  na Uganda hivyo bado tuna kazi ya kuendelea kuchukua tahadhari.

Wale ambao walifanya usajili kwa umakini na kwa kufuata mapendekezo ya benchi la ufundi wameweza kufanya kile ambacho kilikuwa kinahitajika.

Kutokana na maandalizi pamoja na usajili ninaweza kusema ni ngumu kuamini kwamba ushindani utakuwa mdogo hilo sioni kwa msimu huu.

Itapendeza ushindani ukiendelea mpaka mwisho wa ligi kwa kuwa kila mmoja anahitaji kuona timu inapata matokeo chanya. Matokeo mazuri yanatafutwa kwa kufanya kazi na kufanya maandalizi mazuri.

Timu zote ambazo zimefanya usajili kwa mapendekezo yao binafsi wakati wa kujua masuala hayo ni sasa.  Mchezo wa mpira hauhitaji mambo mengi zaidi ya vitendo na data ambazo zinaongea ukweli muda wote.

 Dakika 90 ni muda sahihi na unatosha kuaminisha mashabiki na wanachama wa timu kwamba huyo aliyeletwa ndani kucheza ni pendekezo la kocha ama kiongozi.

Sababu moja kubwa itakayofanya atambulike kwamba alisajiliwa kwa presha ama chaguo la kiongozi ni muda wake atakaoutumia ndani ya uwanja na kile ambacho atakionyesha pia pale atakapopata muda.

Ipo wazi kwamba kuna wale wachezaji ambao walipata nafasi ya kusajiliwa kwa msimu wa 2019/20 ndani ya timu mbalimbali hawakuwa na nafasi kwenye timu zao mpaka msimu unaisha.

Rekodi zinaonyesha kwamba wapo wachezaji ambao walisajiliwa na timu kwa msimu wa 2019/20 na hawajacheza mchezo hata mmoja ndani ya ligi zaidi ya kuishia benchi.

Kwa sasa wachezaji hao wengi wametolewa kwa mkopo na maisha yanaendelea huko waliko wakivinoa viwango vyao ili kufikia pale ambapo benchi la ufundi linahitaji.

Hii ni mbaya na inatoa picha kwamba hakukuwa na chaguo la mchezaji huyo ndani ya kikosi, pia inaua uwezo wa mchezaji na kurudisha nyuma maendeleo ya soka hasa ikiwa alichukuliwa kutoka kwa timu ambayo ilikuwa inahitaji huduma yake labda kutokana na uchumi kuyumba wakashindwa kubaki na mchezaji.

Kwa viongozi wa timu pia ni somo kwamba mpira wa sasa unahitaji fedha na uwekezaji mkubwa hivyo wanajukumu la kuongeza vyanzo vyao vya mapato ili kuweza kubaki na wachezaji ambao wanawahitaji pale msimu unapokwisha.

SOMA NA HII  ROBERTINHO ATAMBA AWAPA NENO HILI MASHABIKI

Tukiachana na timu, mchezaji kwa sasa ana kazi ya kutimiza majukumu yake kwa usahihi ndani ya uwanja ili kurejesha imani kwa mashabiki ambao wanawaamini.

Kwa kuwa maisha ya soka lazima yaendelee mchezaji mmoja kuondoka na kwenda katika timu nyingine hilo halizuiliwi.

Kwa kuwa tayari ligi imeshaanza basi ni muhimu kuona kwamba kila mmoja anapaswa kutimiza majukumu yake ipasavyo hii itafanya ushindani kuwa imara na bora.

Muda ule wa maandalizi ambao ulikuwa ni maalumu kwa ajili ya kujiweka sawa umekwisha na sasa ni muda wa kufanya kazi kwa vitendo bila kuchoka.

Rai yangu kubwa hasa kwa waamuzi ambao ni sehemu ya mchezo na mafanikio ya mpira wetu wanapaswa wasipepese macho katika kazi yao ndani ya uwanja.

Kufanya kwao vizuri ni hazina kwa ajili ya bingwa ambaye atapatikana hapo baadaye kwa kuwa ana kazi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa hivyo atakwenda kufanya vema kwa kuwa hajabebwa.

Ipo wazi kwamba, waamuzi ni binadamu na makosa yapo lakini haipaswi iwe kila siku wao wanabebeshwa zigo la lawama kila baada ya mchezo kuiisha hii haifai.

Kusimamia kwao majukumu ambayo wamepewa kwa uzuri kutaongeza ule ushindani kufanya kila timu kupata ushindi baada ya dakika 90 bila kuwa na sehemu ya kushusha lawama.     

Kila timu kwa sasa inahitaji pointi tatu muhimu hilo lipo wazi na kwa namna mambo yanavyokwenda hivi ndivyo inatakiwa kuwa mpaka mwisho wa msimu.

Bado kwa sasa kumekuwa na malalamiko ambayo yanatolewa hilo huwezi kukwepa lakini ikiwa waamuzi wataamua kufanya kweli inawezekana. Kufuata sheria 17 na kufanya maamuzi sahihi ni tiba tosha kwa haya malalamiko ambayo yamekuwa yakiskika kutoka kwa viongozi.

Tunataka kuona kila timu inafanya maajabu na kupata matokeo mazuri kwenye mechi zote ambazo watacheza iwe nyumbani ama ugenini muhimu kupambana kupata matokeo.

Muda wa kufikiria kuhusu waamuzi kwa sasa usipewe nafasi na badala yake ni lazima kila timu ipambane. Kwa waamuzi wao kazi yao ni moja kusimamia sheria 17 za mpira hakuna jambo jingine.

Mashabiki wenu mtambue kwamba wanajua yapo matokeo matatu, kufungwa, sare na kushinda. Furaha yao kubwa ipo kwenye kushinda basi pambaneni kuwapa mashabiki kile ambacho wanahitaji.

Msimu huu tunahitaji kuona kwamba kila mchezaji, shabiki mpaka benchi la ufundi baada ya mchezo kuisha wanachekelea kwa kuwa wamepata kile wanachostahili.